Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi Ethiopia sasa wanaweza kufanya kazi!

Wakimbizi Ethiopia sasa wanaweza kufanya kazi!

Pakua

Ethiopia imeingia katika historia kufuatia kitendo chake cha kupitisha sheria mpya inayoruhusu wakimbizi kufanya kazi na pia kupata huduma muhimu za kijamii, hatua ambayo imepongezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,UNHCR.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini  Geneva, Uswisi imesema sheria hiyo mpya iliyopitishwa na Bunge la Ethiopia jana tarehe 17 mwezi huu wa Januari imefanya nchi hiyo kuwa na sheria endelevu zaidi barani Afrika kuhusu wakimbizi.

Mathalani sheria hiyo inawezesha wakimbizi kupata vyeti vya kuzaliwa na ndoa pamoja na huduma za kitaifa za fedha kama vile benki na pia kupata elimu na leseni ya udereva.

Kamishna Mkuu wa wakimbizi duniani, Filippo Grandi amenukuliwa akisema, “kupitishwa kwa sheria hii ya kihistoria ni hatua muhimu ya Ethiopia katika historia yake ya siku nyingi ya kukaribisha wakimbizi kwa miongo kadhaa sasa.”

Amesema kwa kuruhusu wakimbizi kutangamana na jamii, Ethiopia inakuwa inatekeleza wajibu wake wa kimataifa kwa wakimbizi na pia kuonyesha mataifa mengine muundo bora zaidi wa kuhifadhi wakimbizi.

Hatua  ya Ethiopia ya kubadili sheria  yake kuhusu wakimbizi inakuja siku chache baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Matifa kupitisha tarehe 17 mwezi  uliopita wa Disemba, Mkataba wa Kimataifa wa wakimbizi.

Ethiopia hivi sasa inahifadhi zaidi ya wakimbizi 900,000, idadi kubwa wakitoka Sudan Kusini, Somalia, Sudan na Eritrea na idadi kidogo kutoka Yemen na Syria.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Grace Kaneiya
Audio Duration
1'29"
Photo Credit
© UNHCR/Diana Diaz