Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya CAR na vikundi vilivyojihami kukutana Sudan mwezi huu

Serikali ya CAR na vikundi vilivyojihami kukutana Sudan mwezi huu

Pakua

Mazungumzo  yenye lengo la kurejesha amani ya kudumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR sasa yatafanyika tarehe 24 mwezi huu huko nchini Sudan. 

Juhudi za kuzindua tena mashauriano kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR na vikundi vilivyojihami, zimeleta pamoja mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix na kamishna wa amani na usalama wa Muungano wa Afrika, Smail Chergui ambao wamekuwa na mazungumzo na Rais Faustin Archange Touadéra na wawakilishi wa serikali hiyo mjini Bangui.

Baada ya majadiliano yao wamezungumza na waandishi wa habari ambapo rais Touadéra ametangaza kuwa  mazungumzo kati ya serikali na vikundi vilivyojihamini yenye lengo la kuleta amani ya kudumu nchini humo yatafanyika tarehe 24 mwezi huu mjini Khartoum nchini Sudan.

Bwana Lacroix ameelezea kuunga mkono kuzinduliwa kwa mashauriano akisema kuwa.

Mwaka huu ni lazima uwe mwaka ambao mashauriano,  ujenzi wa amani, utulivu na maridhiano lazima viwepo.”

Mashauriano hayo ambayo yanaratibiwa na Muungano wa Afrika ni habari njema kwa   watoto wengi ambao walilazimishwa kujiunga na vikundi vya waasi akiwemo kijana Ahmed ambaye anahofia maisha yake baada ya kukimbia waasi na sasa anahifadhiwa na polisi mjini Bangui.

“Wananiita msaliti, ndio maana  walinifunga na kunigonga, nipo hapa kwa ajili ya usalama wangu. Tangu niwasili hapa polisi wamenitunza vizuri, waliwasiliana pia na MINUSCA ambao waliniangalia vizuri”

MINUSCA ni ujumbe wa Umoja wa  Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, nchi ambayo tangu mzozo uanze mwaka  2013 watoto kadhaa wametumikishwa jeshini.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'41"
Photo Credit
MINUSCA