Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twashona nguo, twafuga, umaskini kwaheri- Wanufaika wa mradi wa Benki ya Dunia Afghanistan

Twashona nguo, twafuga, umaskini kwaheri- Wanufaika wa mradi wa Benki ya Dunia Afghanistan

Pakua

Mradi wa Benki ya Dunia na serikali ya Afghanistan wa kuhamasisha wanakijiji kujitegemea kupitia biashara ndogo umewezesha jamii kujikwamua kiuchumi na kijamii.

Mradi huo unatekelezwa katika majimbo matano kati ya 34 ya Afghanistan ambapo mojawapo ni jimbo la Nangarhar ambalo hali yake ya kiuchumi imekuwa ikidorora kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi.

Miongoni mwa wanufaika ni Mullah Khan ambaye miaka mitatu iliyopita ufukara ulikuwa umeota mizizi kwenye kaya yake.

Hata hivyo baada ya kupata mtaji wa takribani dola 900 kutoka chama cha kuweka na kukopa cha kijijini kwao kinachopata fedha kutoka Benki ya Dunia na taasisi ya Afghanistan, sasa anaweza kununua mbegu bora na mbolea.

(Sauti ya Mullah Khan)

“Mazao niliyokuwa nauza zaidi ni vitunguu swaumu na giligilani. Nilikuwa napata dola zaidi ya 2500. Niliweza kurejesha mkopo na iliyosalia  nilijenga uzio kwenye shamba langu kuzuia watoto na mifugo.”

Mradi huu unaolenga kuhamasisha wakazi wa vijijini kuweka akiba na kutumia fedha kujikwamua kiuchumi, umenusuru pia familia ya Bi. Nazeema, mama wa watoto 6 na mwenye mume mgonjwa.

Mkopo aliopata alitumia kununua cherehani na ng’ombe mmoja ambapo sasa katika kila wiki mbili anashona nguo 150 na kuziuza kwenye soko la kijiji, huku ng’ombe akiwapatia maziwa  yanayotumiwa na familia.

Mradi huu umenufaisha zaidi ya wakazi 21, 000 kijijini Nangarhar, na umeboresha maisha ya wanakijiji na kuongeza vipato vyao.

 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Siraj Kalyango
Audio Duration
1'41"
Photo Credit
Ufugaji nchini Somalia hususan maeneo ya kusini uko mashakani kutokana na mafuriko yaliyokumba eneo hilo karibuni. (Picha:FAO)