Rasimu ya sheria Denmark ya kunyang’anya vifaa wasaka hifadhi yatia wasiwasi

Rasimu ya sheria Denmark ya kunyang’anya vifaa wasaka hifadhi yatia wasiwasi

Pakua

Leo kwenye baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi, nchi wanachama wamejadili hali iliyoko nchini Denmark ikiwemo sheria mpya inayotarajiwa kupitishwa na bunge la taifa hilo kuhusu wasaka hifadhi.

Sheria hiyo ikipitishwa itaruhusu mamlaka za serikali kuchunguza vifaa binafsi vya wasaka hifadhi wanapoingia nchini humo, na kuwanyang’anya pesa au vifaa venye thamani ya zaidi ya dola 1,500.

Kwenye hotuba zao wakati wa mkutano huo Mwakilishi wa Misri Mohamed Elmolla na Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye baraza la Haki za Binadamu Balozi Keith Harper wameelezea wasiwasi wao kuhusu rasimu ya sheria hiyo, Balozi Harper akisema

(Sauti ya Balozi Harper)

“Wakati ambapo Marekani inatambua ongezeko la shinikizo kwa rasimali za fedha na usalama za Denmark na nchi zingine za Ulaya lililosababishwa na mzozo wa wakimbizi na wahamiaji, tuna wasiwasi kuhusu rasimu ya sheria inayotarajiwa kupitishwa na bunge la taifa ambayo itaruhusu serikali ya Denmark kuchunguza vifaa vya wasaka hifadhi na kuchukua pesa na vifaa venye thamani.”

Kwa upande wake, Waziri wa mambo ya nje wa Denmark Kristian Jensen amesikitishwa na wasiwasi huo akisema umesababishwa na sintofahamu kubwa, akieleza kwamba lengo ni kufadhili huduma zitakazotolewa kwa ajili ya wakimbizi, na pia vifaa venye thamani ya kibinafsi kama vile pete za ndoa havitachukuliwa.

Photo Credit
Wasaka hifadhi wakaguliwa na polisi nchini Macedonia. Picha ya UNICEF/Gjorgji Klincarov