Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maziwa ya mama ni muhimu kwa mustakbali wa mtoto

Maziwa ya mama ni muhimu kwa mustakbali wa mtoto

Jinsi akina mama wenye shughuli nyingi wanavyoweza kufanikisha unyonyeshaji wa pekee

Wiki ya kimataifa ya mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama ikiwa imefikia tamati jana Alhamisi leo tunakupeleka nchini Tanzania kusikia ushuhuda wa mama aliyetekeleza wito wa mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya, WHO na la kuhudumia watoto wa kunyonyesha watoto wao maziwa yao kwa kipindi kirefu. Msimulizi wako ni Cecily Kariuki.

(Taarifa ya Cecily Kariuki)

Simulizi yangu inajikita kwenye chapisho la UNICEF Tanzania kwenye mtandao wa X, zamani Twitter likimuangazia Noela, afisa msaidizi wa shirika hilo akiwa nyumbani kwake na watoto wake akiwemo mtoto mchanga.

(Sauti ya Noela)

“Huyu ni binti yangu Zoey na huyu ni binti yangu Chrissete, Zoey nimejifungua mwezi Januari na mpaka leo nimeweza kumnyonyesha kwa muda wa miezi sita”

Kwanini Noela aliamua kufanya hivyo?

(Sauti ya Noela)

Nilifanya maamuzi haya kwa sabau niliona yana faida nyingi kwangu mimi na kwa mtoto. Faida mojawapo  ilikuwa ni kwamba kiafya mtoto angepata afya njema, angepata lishe kamili, pia ningemkinga na magonjwa mbalimbali.”

WHO na UNICEF wanasema kunyonyesha watoto hakupunguzi tu mzigo wa magonjwa ya utotoni, bali pia hatari za aina fulani za saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa mama.

Lakini je, Noela anapoenda kazini au anaposafiri, anafanya nini ili kuhakikisha mwanawe anayapata maziwa ya mama?

(Sauti ya Noela)

“Endapo nakuwa sipo nyumbani, au nimepata dharura ya kuenda mahali, huwa ninatumia mashine kama hii kukamua maziwa yangu na kuyahifadhi, baadaye msaidizi humpa mtoto maziwa ya mama. Kwa hiyo hata niwapo nje ya nyumbani  nakuwa na uhakika binti yangu anapata maziwa ya mama.”

Noela akiwa ameshikilia pampu ya kukamua maziwa anatoa ushauri kwa akina mama wanaolazimika kuwa mbali na watoto wao kwa sababu mbalimbali.

(Sauti ya Noela)

“Unapokua na kifaa kama hichi unaweza kukamua na kuhifadhi maziwa kwa muda mrefu kwenye friji ili mtoto aweze kupata maziwa baadaye. Maziwa ya mama yana faida kubwa sana kwa mtoto huvyo nawashauri wamama wote wajitahidi kufanya zoezi la unyonyeshaji

Pakua
Audio Credit
UN News/ Cicely Kariuki
Audio Duration
1'54"
Photo Credit
© UNICEF/Donaig Le Du