Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yafanikisha miradi ya kusaidia jamii nchini Somalia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

FAO yafanikisha miradi ya kusaidia jamii nchini Somalia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Pakua

Huku takriban watu milioni 7 nchini Somalia wakihitaji msaada wa kuokoa maisha mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO linahimiza jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono Wasomali wanaokabiliwa na athari za njaa,mabadiliko ya tabianchi, migogoro na kufurushwa makwao. 

FAO sio kwamba wao wanahimiza wengine kusaidia wasomali, bali wao pia na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa wanatekeleza miradi mbalimbali yakuwasaidia wananchi wa Somalia hususan katika kuhakikisha wana uhakika wa kujipatia chakula na kupunguza athari za vichocheo muhimu vya uhaba wa chakula ambavyo ni kama vile mafuriko, ukame, bei juu za chakula pamoja na migogoro.

Programu zinazotekelezwa ni pamoja na kuboresha kinga na kujiandaa kwa majanga ya chakula katika jamii za vijijini, kuimarisha uzalishaji wa mifugo, na kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu kilimo kinachozingatia hali ya hewa.

Bi. Edeba Ali Hassan (33), ni mkulima aliyelazimika kukimbia huko Bakool kutokana na machafuko na kuhamia Dolow, ni mnufaika wa programu iitwayo Mpango wa Hatua za Pamoja za Ustahimilivu – JOSP unaotekelezwa na FAO kwa ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Bi. Edeba anasema programu hiyo imempatia fedha taslimu, pembejeo za kilimo kwa misimu miwili, amepewa shamba pamoja na mfumo wa umwagiliaji unaotumia nishati ya jua.

“Nina watoto 10, na siwezi kuwahudumia kwa sababu hakuna kazi isipokuwa kilimo, ndiyo maana nilijiunga na Mpango wa Pamoja wa Ustahimilivu.”

Alexander Jones, Mkurugenzi, Idara ya Uhamasishaji Rasilimali wa FAO anasema programu wanazozitekeleza nchini Somalia zinalenga zaidi kusaidia watu katika kupata uhakika wa chakula katika maeneo ambayo mara kwa mara yanaathiriwa na ukame na mafuriko.

“Mradi wa JOSP unasaidia kukarabati eneo kubwa lenye takriban wanufaika milioni 1.5 kupitia usimamizi wa maji, kupitia programu za kijamii za maji, kwa ajili ya maeneo yanayoathirika na mafuriko na ukame.”

Mpango huu mkubwa wa kuleta mabadiliko nchini Somalia unatekelezwa kwa ufadhili kutoka kwa Ubalozi wa Uingereza mjini Mogadishu, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kujenga Amani (UNPBF), pamoja na michango inayotarajiwa kutoka kwa shirika la Marekani la misaada ya maendeleo USAID na Mfuko wa Pamoja wa Somalia (SJF).

Audio Credit
Leah Mushi
Sauti
1'55"
Photo Credit
©FAO/Arete/Abdulkadir Zubeyr.