Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaomba msaada wa haraka kusaidia wakimbizi kutoka Sudan wanaoingia nchini Chad

Wakimbizi wa Sudan wakisubiri kupokea chakula huko Adre, karibu na mpaka wa Chad na Sudan.
© UNHCR/Nicolo Filippo Rosso
Wakimbizi wa Sudan wakisubiri kupokea chakula huko Adre, karibu na mpaka wa Chad na Sudan.

UNHCR yaomba msaada wa haraka kusaidia wakimbizi kutoka Sudan wanaoingia nchini Chad

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, linatoa wito kwa msaada wa haraka wa kimataifa huku janga la kibinadamu mashariki mwa Chad likifikia hatua mbaya.

Akizungumza na waaandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi, Mwakilishi wa UNHCR nchini Chad Laura Lo Castro ametoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa akisema kuwa theluthi moja ya wakimbizi wapya bado wako katika hali mbaya kwenye maeneo yasiyo rasmi kando ya mpaka na mji wa Adre.

Adre, mji uliokuwa na watu 40,000 hapo awali, lakini kwasasa unapata shida kuhudumia ongezeko la wakimbizi ambalo ni mara sita zaidi.

“Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi wa Sudan katika maeneo ya mpakani, matatizo ya kiafya na matukio ya usalama yanayozidi kuongezeka na msimu wa mvua unaokaribia, hatua za haraka zinahitajika.” Anaonya mwakilishi huyu.

Kwa mujibu wa UNHCR, hali ya dharura nchini Chad inachangiwa na mapigano makali katika eneo la Darfur nchini Sudan. Licha ya juhudi za mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika kusaidia mwitikio wa dharura wa Serikali, hali inazidi kuwa mbaya kwa haraka.

"Hali ya msongamano na usafi duni huko Adre imesababisha mgogoro mkubwa wa afya, na zaidi ya wagonjwa 1,200 wa homa ya Ini - Hepatitis E wameripotiwa, ikiwemo vifo vitatu." Anasema Lo Castro.

Anatoa tahadhari kuwa msimu wa mvua unaotarajiwa kuanza kati ya mwezi Juni na Septemba, utazidisha mgogoro, na huenda kusababisha milipuko ya magonjwa yaenezwayo kwa maji kama vile kipindupindu na kuzuia upatikanaji wa huduma za kibinadamu.

Ombi la UNHCR la 2024 kwa msaada mashariki mwa Chad halijafadhiliwa vya kutosha na ni asilimia 10 pekee ya dola milioni 214.8 zilizohitajika zimepatikana hadi sasa.

Lo Castro anabainisha kuwa ili kufanikisha mahitaji ya haraka, UNHCR inahitaji dola milioni 80 kwa dharura ili kujenga maeneo matatu zaidi yenye huduma na miundombinu muhimu ili waweze kuwahamisha wakimbizi wapya 150,000 kutoka hali ya msongamano na isiyo na usafi na kuwapatia msaada wa kuokoa maisha ikiwemo makazi, chakula, maji safi, na huduma za afya na elimu.

Kwa mujibu wa Lo Castro, kuna hatari kubwa ya uhamishaji zaidi kwani mapigano yanaendelea katika mji wa El Fasher na maeneo ya vijijini yanayozunguka eneo hilo huko Kaskazini mwa Darfur.

Vitendo vya uporaji na uchomaji wa vijiji pamoja na njaa inayotarajiwa nchini Sudan itasababisha wakimbizi zaidi kuingia Chad.

Mama mkimbizi wa Sudan na mwanawe wanatafuta hifadhi katika makazi ya muda huko Hilouta, Chad.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Mama mkimbizi wa Sudan na mwanawe wanatafuta hifadhi katika makazi ya muda huko Hilouta, Chad.

Tayari kuna juhudi zimefanyika

UNHCR na wadau wake wameongeza maeneo sita ya wakimbizi, na kujenga vijiji viwili kwa ajili ya wakimbizi wa Chad waliorejea. Maeneo haya yana huduma muhimu na miundombinu, ikiwemo makazi ya familia, kliniki za muda, vituo vya maji, vifaa vya usafi na elimu vinavyojulikana kama maeneo ya kujifunzia kwa muda.

Hata hivyo, Lo Castro anatahadharisha kuwa juhudi hizi hazitoshi kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo.

Ziara ya pamoja ya ufuatiliaji iliyofanywa na mshirika wa serikali na UNHCR katika kituo cha kuingia mpakani cha Tine huko Wadi Fira ilithibitisha wakimbizi wapya 300 waliowasili katika wiki za hivi karibuni, huku wakimbizi wakiripoti safari za kutisha za hadi siku 15 kuepuka wanamgambo nchini Sudan.

UNHCR inasisitiza wito wake kwa pande zote kuruhusu raia wanaotaka kusafiri ndani na nje ya El Fasher kwenda maeneo salama kufanya hivyo.

Katika muktadha huu, Serikali ya Chad imeomba kwa dharura UNHCR na washirika kuharakisha uhamisho wa wakimbizi wapya kutoka maeneo ya mpakani, hasa kutoka Adre. UNHCR imejibu kwa kufungua eneo jipya kuhudumia hadi watu 50,000, lakini zaidi inahitajika.