Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasudan wangapi wafe ndio pande kinzani Sudan ziache kupigana? Ahoji Türk

Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)
© UNICEF/Shehzad Noorani
Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)

Wasudan wangapi wafe ndio pande kinzani Sudan ziache kupigana? Ahoji Türk

Haki za binadamu

Nimeshtushwa sana, kwa mara nyingine na ripoti za muaji ya kikatili ya raia kwenye kijiji cha Wad Al-Noura jimboni al Jazira nchini Sudan, Ndivyo ilivyoanza taarifa ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa haki za binadamu Volker Türk iliyotolewa leo Geneva, USwisi ikijielekeza kwenye tukio hilo la Jumatano lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 100.

Shambulio hilo limefanywa na wanamgambo wa Rapid Support Forces, au RSF ambao wanapigana na jeshi la serikali la Sudan, SAF tangu kuanza kwa mapigano tarehe 15 mwezi Aprili mwaka jana wa 2023 kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum, mapigano ambayo sasa yamesambaa takribani nchini kote.

RSF walitumia silaha nzito

“Taarifa kutoka ofisi yangu zinadokeza kwamba RSF walitumia silaha zinazosambaa maeneo mengi, ikiwemo makombora mazito,” amesema Bwana Türk  kwenye taarifa hiyo akiongeza kuwa mapigano pia yaliibuka kati ya RSF na watu waliohamasishwa na SAF.

“Mauaji haya yanaongezea kwenye shaka na shuku zangu kubwa ya iwapo katika vita hii kanuni za kivita za kutumia silaha kulingana nae neo na pia kutofautisha maeneo, zinazingatiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Amesema mashambulio hayo yanaibua hoja ya kuwapatia silaha vikundi vya kijamii kwa lengo la kuendeleza chuki.

Ametoa wito kwa RSF na pande zote husika kufanya uchunguzi wa haraka wa tukio hilo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

“Waliohusika na mauaji haya kinyume cha sheria wawajibishwe. Ni idadi ipi ya wasudan wanaouawa inapaswa kufikiwa kabla ya pande husika kwenye vita hii zitaacha kupigana?” amehoji Bwana Türk.

Mjumbe wa Katibu Mkuu anaendelea na juhudi za kushirikisha pande zote

Mapema Alhamisi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake alilaani vikali shambulio hilo huku akitaka pande kinzani zijiepushe na mashambulizi yanayoweza kuumiza raia au kuharibu miundombinu ya kiraia.

Kwa sasa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kwa Sudan, Ramtane Lamamra anaendelea kushirikisha pande zote ili kusongesha juhudi za amani nchini humo, imesema taarifa hiyo ikitamatisha kwa Katibu Mkuu kusema ,Umoja wa Mataifa unasalia umejizatiti kusaidia juhudi za usuluhishi za kimataifa na kufanya kazi na pande zote husika ili kumaliza mzozo huo.