Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei ya chakula duniani imepanda kwa mwezi wa tatu mfululizo, nafaka na maziwa vikishika usukani: FAO

Bei ya nafaka inapanda kimataifa.
© WFP/Michael Tewelde
Bei ya nafaka inapanda kimataifa.

Bei ya chakula duniani imepanda kwa mwezi wa tatu mfululizo, nafaka na maziwa vikishika usukani: FAO

Tabianchi na mazingira

Bei za vyakula duniani zimepanda kwa mwezi wa tatu mfululizo mwezi Mei, asilimia kubwa ikiwa katika ongezeko la gharama ya nafaka na bidhaa za maziwa lilizidi kupungua kwa bei ya sukari na mafuta ya mboga kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.

Tathimini ya bei ya chakula ya FAO, ambayo hufuatilia mabadiliko ya kila mwezi ya gharama ya bidhaa kuu za chakula duniani kote, ilikuwa pointi 120.4 mwezi Mei, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.9 kutoka mwezi Aprili, lakini asilimia 3.4 chini ya kiwango cha mwaka mmoja uliopita na asilimia 24.9 chini ya kilele kilichorekodiwa mwezi Machi 2022.

Bei ya nafaka

Tathimini hiyo inasema bei ya nafaka iliongezeka kwa asilimia 6.3 ikilinganishwa na mwezi Aprili. Hii iliungwa mkono na kupanda kwa bei ya ngano duniani kote, ikionyesha wasiwasi unaoongezeka kuhusu hali mbaya ya mazao katika kanda muhimu zinazozalisha nafaka hiyo. 

Bei za mauzo ya mahindi pia zimeelezewa kupanda, zikisukumwa na matatizo ya uzalishaji nchini Ajentina kutokana na ugonjwa wa Spiroplasma na nchini Brazili kutokana na hali mbaya ya hewa, pamoja na shughuli chache za mauzo nchini Ukraini. 

Na kwa upande wa tathimini ya bei ya mchele iliongezeka kwa asilimia 1.3 mwezi Mei.

Nyama, maziwa na sukari

Tathimini ya bei ya maziwa inaonyesha ilipanda kwa asilimia 1.8 kutoka mwezi Aprili, ikishajihishwa na kuongezeka kwa mahitaji kabla ya likizo ya majira ya joto na matarajio ya soko kwamba uzalishaji wa maziwa katika eneo la Ulaya Magharibi unaweza kushuka chini ya viwango vya kihistoria. 

Mahitaji mapya ya uagizaji bidhaa kutoka kwa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini pia yalichangia kupanda kwa bei ya bidhaa za maziwa.

Na bei ya sukari ilishuka kwa asilimia 7.5 kuanzia Aprili, hasa kutokana na mwanzo mzuri wa msimu nchini Brazili. 

Bei ya chini ya mafuta ghafi duniani pia imeweka shinikizo kwa bei ya sukari, na hivyo kupunguza mahitaji.

Kwa upande wa bei ya mafuta ya mboga, ilipungua kwa asilimia 2.4 ikilinganishwa na Aprili.

Nayo bei ya nyama FAO inasema ilishuka kwa asilimia 0.2, na bei za kimataifa za kuku na ng'ombe zikianguka huku mayai na nyama ya nguruwe zikipanda.

Utabiri wa msimu ujao

Leo pia, FAO imetoa utabiri wake wa kwanza wa msimu wa mwaka 2024-25, ikitoa wito kwa uzalishaji wa nafaka duniani kufikia tani milioni 2,846, kulingana na rekodi ya uzalishaji ya 2023-24. 

Uzalishaji wa kimataifa wa mahindi na ngano unakadiriwa kupungua, huku uzalishaji wa shayiri, mpunga na mtama ukitarajiwa kuongezeka. 

Hali mbaya ya hewa ya hivi karibuni katika eneo la Bahari Nyeusi huenda ikapunguza uzalishaji wa ngano duniani.

Jumla ya matumizi ya nafaka duniani yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 0.5 mwaka 2024-25 hadi rekodi mpya ya juu ya tani milioni 2,851, ikisukumwa na kuongezeka kwa matumizi ya chakula, hasa mchele.

Hifadhi ya nafaka ya kimataifa huenda ikaongezeka pia kwa asilimia 1.5 kutoka viwango vyake vya mwanzoni mwa mwaka, na kufikia rekodi ya tani milioni 897. Hesabu za mahindi, shayiri, mtama na mchele zinatarajiwa kuongezeka, huku akiba ya ngano ikapungua.

FAO inakadiria kuwa biashara ya nafaka duniani itashuka kwa asilimia 1.3 mwaka baada ya mwaka hadi kufikia tani milioni 481, ikichochewa na matarajio duni ya biashara ya mahindi. 

Biashara ya kimataifa ya mchele nayo inakadiriwa kukua kwa kasi.