Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO wa dola milioni 17 kusaidia wakulima nchini Ukraine

Svitlana kutoka eneo lililoathiriwa na migogoro mashariki mwa Ukraine alipokea kuku wa siku 30 kwa ajili ya ufugaji wa aina mbili.
© FAO/Viktoriia Mykhalchuk
Svitlana kutoka eneo lililoathiriwa na migogoro mashariki mwa Ukraine alipokea kuku wa siku 30 kwa ajili ya ufugaji wa aina mbili.

Mradi wa FAO wa dola milioni 17 kusaidia wakulima nchini Ukraine

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika kushughulikia kupanda kwa bei za vyakula duniani kote shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limezindua mradi wa dola milioni 17 wa kusaidia wakulima nchini Ukraine ili kuokoa mavuno yao katika kipindi cha mwezi huu wa Julai na ujao wa Agosti huku wakihakikisha uuzaji wa mazao nje ya nchi. 

Ukraine ni moja ya nchi tano zinazoongoza kwa mauzo ya mazao ya nafaka katika masoko ya kimataifa duniani ambapo inasambaza zaidi ya tani milioni 45 za nafaka kila mwaka na hivyo vita nchini humo imesababisha uhaba wa mazao na kupanda kwa bei. 

Mradi huo uliofadhiliwa na Japan unalenga kuisaidia wizara ya Kilimo na Chakula ya Ukraine kurejesha uwezo wa kuhifadhi nafaka na kuimarisha mnyororo wa ugavi kuanzia kwenye mavuno hadi kupeleka nje ya nchi na pia kudumisha uwezo wa uzalishaji wa wakulima nchini humo ili kuweza kuendelea na uzalishaji katika siku zijazo. 

Mkurugenzi wa Ofisi ya dharura na ustahimilivu wa FAO Rein Paulsen ameseme “Wakulima wa Ukraine sio tu wanalima chakula kwa ajili yao wenyewe na jamii zao lakini pia wanalisha mamilioni ya watu duniani kote na hivyo kuhakikisha wanaweza kuendelea na uzalishaji, kuhifadhi kwa usalama na kupata masoko mbadala ya kuuza mazao yao ni muhimu ili kupata uhakika wa upatikanaji wa chakula, kulinda Maisha , kuimarisha upatikanaji wa chakula nchini humo Pamoja na kuhakikisha nchi nyingine zinazotegemea uagizaji wa bidhaa zinakuwa na usamabaji thabiti na wakutosha wa nafaka kwa ghrama zinazoweza kudhibitiwa.”

Cabo Verde inakabiliwa na viwango vya kuvunja rekodi vya uhaba wa chakula kutokana na ukame, COVID-19 na mzozo wa Ukraine.
WFP/Richard Mbouet
Cabo Verde inakabiliwa na viwango vya kuvunja rekodi vya uhaba wa chakula kutokana na ukame, COVID-19 na mzozo wa Ukraine.

Mazao mengi yapo kwenye maghala

Kutokana na vita inayoendelea nchini Ukraine na kuzibwa kwa bandari nyeusi inayotegemewa na chi hiyo katika kusafirisha chakula nje ya nchi, wizara ya kilimo ya nchi hiyo imesema ina tani milioni 18 za mavuno ya mwaka jana ya nafaka na mbegu za mafuta katika maghala yakisubiri kuuzwa nje ya nchi. 

Njia mbadala ya kutumia reli au kusafirisha kwa njia ya mto kaziwezi kufidia mauzo ya nje yaliyopotea kupitia usafiri wa bahari Pamoja na vikwazo vipya kwenye minyororo ya ugavi ambayo havijatatuliwa. 

Matarajio ya mavuno msimu huu ni kuvuka tani milioni 60 za nafaka lakini kutoka ana kushindwa kuuzwa nje ya nchi mavuno ya mwaka jana nchi hiyo inakosa sehemu ya kuhifadhia mavuno mapya kwakuwa asilimia 30 ya uwezo wake ungali na mazao yam waka jana.

Mkuu wa FAO nchini Ukraine Pierre Vauthier amesema kupitia mradi huu uliofadhiliwa na Japan watawafikia wakulima katika mikoa kumiiliyoko mashariki, katikati, kusini na kaskazini mwa nchi hiyo.
“FAO tutaweza kushughulikia suala la uhifadhi wa mazao kwa kutoa magunia kuweka nafaka, machine za kupakua na kupakia nafaka kutoka kwa wakulima wadogo na kuhifadhi katika kontena za kawaida za kuhifadhi kwa wazalishaji na vyama vya ukubwa wa kati.” Amebainisha Vauthier

Ameeleza pia mradi huo utatoa msaada wa kitaalamu kwa seriklai ya Ukriane ili kuendesa njia mbadala za usafirishaji wa nafaka nje ya nchi na kukuza upanuzi wa haraka wa uwezo wa kiufundi katika maabara ya Lzmail, ambayo ni kituo cha kuwawezesha wakulima kupima iwapo wamefikia viwango vya kimataifa vya usalama wa mifugo na chakula na kisha kupatiwa cheti cha uthibitisho.