Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu mil 33 wanahitaji msaada wa kuokoa maisha katika Ukanda wa Sahel

Wanufaika wa programu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP ya kugawa msaada wa chakula chenye lishe kwenye kijiji kimoja eneo la Zinder nchini Niger
© WFP/Simon Pierre Diouf
Wanufaika wa programu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP ya kugawa msaada wa chakula chenye lishe kwenye kijiji kimoja eneo la Zinder nchini Niger

Takriban watu mil 33 wanahitaji msaada wa kuokoa maisha katika Ukanda wa Sahel

Msaada wa Kibinadamu

Maisha ya watu milioni 32.8 katika eneo zima la Ukanda wa Sahel wameathiriwa na mchanganyiko wa majanga mbalimbali ambayo yanazidisha ukosefu wa utulivu na kuzorotesha hali ya usalama na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwafanya watu wengi kuwa tegemezi wa msaada wa kibinadamu na huduma za ulinzi. 

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA kutoka Dakar Senegal imeonya kuwa maisha ya watu hao yapo hatarini isipokuwa pale tu watoa misaada ya kibinadamu wanapopatiwa misaada ya rasilimali zinazohitajika kukabiliana na majanga hayo na kusaidia watu walio hatarini zaidi katika ukanda huo. 

Mkuu wa OCHA katika Ukanda huo Bwana Charles Bernimolin ametaja maeneo ambayo mgogoro huo ni hatari zaidi kuwa ni pamoja na Pwani ya nchi ya Benin, Côte d'Ivoire, Ghana na Togo ambazo zinajumla ya wasakahifadhi 123,116 wakati nchi ya Mauritania imewakaribisha wasakahifadhi 128,100. 

Akizungumzia juu ya ripoti ya Muhtasari wa Mahitaji na Mahitaji ya Kibinadamu wa 2024 kwa Ukanda wa Sahel,iliyojikita kuangazia hali ya migogoro ya kibinadamu wanayokabiliana nayo na inamaanisha nini kwa watu wanaoishi katika ukanda huo pamoja na namna wafadhili wa kibinadamu wanavyokabiliana na majanga hayo Bwana Bernimolin amesema 

“Wasaidizi wa kibinadamu kote katika Ukanda wa Sahel wanafanya kazi nzuri sana na  mara nyingi katika mazingira magumu zaidi. Lakini mchanganyiko wa migogoro wanayokabiliana nayo ni ngumu zaidi kuliko hapo awali. Takriban watu milioni 33 katika eneo lote wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. Hata hivyo bila rasilimali zinazohitajika kukidhi mahitaji yao, majanga haya yataendelea kuongezeka na kuenea, na hivyo kumomonyoa ustahimilivu na kuhatarisha maisha ya watoto, wanawake na wanaume,”

Kwa mwaka huu wa 2024 wadau hao wa masuala ya kibinadamu wanahitaji dola bilioni 4.7 ili kukidhi mahitaji ya dharura ya watu milioni 20.9 walioko nchini Burkina Faso, Kaskazini mwa Cameroon, Chad, Mali, Niger, na majimbo ya Adamawa, Borno na Yobe ya Nigeria.

Hata hivyo mwakilishi huyo wa OCHA ameshukuru wafadhili “Shukrani kwa michango ya ukarimu ya wafadhili, wasaidizi wa kibinadamu wanaleta mabadiliko ya kweli katika Sahel. Ninahimiza jumuiya ya kimataifa kutoa zaidi ufadhili ili kuhakikisha mipango ya kukabiliana na misaada ya kibinadamu ya kanda inaweza kutekelezwa kikamilifu.” 

Pamoja na ufadhili Mkuu huyo ameeleza suluhu ya muda mrefu ni  wadau wa kimataifa kuendelea kushirikiana na kanda hiyo, ili kuunda masuluhisho ya kudumu ambayo yatapunguza mahitaji ya kibinadamu katika siku zijazo.

Data izinazokusanywa kuhusu mabadiliko ya tabianchi zinaweza kusaidia kutoa maamuzi kuhusu kilimo, kama inavyoonekana pichani nchini Niger.
© FAO/Giulio Napolitano
Data izinazokusanywa kuhusu mabadiliko ya tabianchi zinaweza kusaidia kutoa maamuzi kuhusu kilimo, kama inavyoonekana pichani nchini Niger.

Hali ikoje Ukanda wa Sahel?

Ukanda wa Sahel unakabiliwa na kuongezeka kwa ghasia na migogoro ambayo inatishia maisha na kulazimisha familia kukimbia makazi yao na kuzuia upatikanaji wa huduma za kimsingi za kijamii - watoto milioni 2.2 wananyimwa haki yao ya elimu kutokana na kufungwa kwa shule, na vituo vya afya 1,263 vimefungwa. 

Ukanda huo ni hifadhi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi milioni mbili na wakimbizi wa ndani milioni 5.6, wengi wao wakiwa wamelazimika kuyahama makazi yao. 

Madhara yanayoongezeka yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi yanazidisha mazingira kuwa magumu. Ulinzi wa maisha ya binadamu na haki za kimsingi na utu wa watu bado ni hitaji la dharura la kibinadamu. Wanawake na wasichana, watoto, na wale walio na mahitaji maalum ni hatari sana. 

Katika msimu ujao wa mwezi Juni-Agosti, watu milioni 16.7 watajitahidi kujilisha wenyewe suala ambalo ni hatari kwa maisha yao kwa kuzingatia mazingira na hali halisi.

Wadau wa misaada ya kibinadamu walitoa msaada wa kuokoa maisha na huduma za ulinzi kwa zaidi ya watu milioni 15.6 kote Sahel mwaka 2023. Hata hivyo, pamoja na mipango ya kukabiliana na misaada ya kibinadamu kwa nchi sita za Sahel kupokea tu asilimia 41 ya ufadhili unaohitajika, mamilioni waliachwa bila msaada muhimu.

Hadi kufikia tarehe 3 Juni 2024, asilimia 16 ya mahitaji ya ufadhili wa kibinadamu ya mipango sita ya kukabiliana na nchi ya 2024 ilitimizwa. Iwapo shughuli za usaidizi zikishindwa kufanya kazi  maisha ya mamilioni ya watu kote Sahel yatakuwa hatarini.