Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya kimataifa ya ‘kabumbu’

Abdirahman Sheuna (mwenye jezi nyekundu) akiwania mpira dhidi ya wachezaji kutoka shule ya msingi ya mtaani kwenye "Tamasha la Kakuma la Kandanda kwa Shule"...
© UNHCR/Samuel Otieno
Abdirahman Sheuna (mwenye jezi nyekundu) akiwania mpira dhidi ya wachezaji kutoka shule ya msingi ya mtaani kwenye "Tamasha la Kakuma la Kandanda kwa Shule"...

Leo ni siku ya kimataifa ya ‘kabumbu’

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya kimataifa ya mpira wa miguu ujulikanao pia kama soka au pia “kabumbu” siku iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 7 mwezi huu wa Mei kwa kutambua mchango wa mchezo huo katika kusongesha amani dunia na pia katika kufanikisha malengo ya Umoja wa Matiafa ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kupitia wavuti wa kuadhimisha siku hii adhimu, Umoja wa Mataifa unasema kuwa michezo zaidi ya kuwa ni sehemu ya burudani, ni lugha inayotumbulika duniani kote ikizungumzwa na watu wa marika yote bila kubagua utaifa, utamaduni, mipaka ya kiuchumi na kijamii. Jambo hili linalopendwa na watu wote linaimarisha jamii na kujivunia kitaifa.”

Umoja wa Mataifa unasema pia kuwa mpira wa miguu pia unasongesha afya na ustawi “na pia umekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha na kujenga usawa wa kijinsia na kuwezesha wanawake na wasichana iwe ndani ya uwanja wa mpira nan je ya uwanja wa mpira.”

Halikadhalika, mpira wa miguu ni kichocheo cha ujumuishwaji wa kijamii, unajenga umoja na kuvunja mipaka kati ya jamii zenye tofauti.

“Mpira wa miguu unatoa fursa ya ambamo kwayo watu kutoka pande tofauti wanakutana na kujenga maelewano ya pamoja, stahmala, heshima na mshikamano,” umesema Umoja wa Mataifa.

Usuli wa siku hii

Mwaka huu wa 2024 ni miaka 100 tangu kuchezwa kwa shindano la kwanza la kimataifa la mpira wa miguu likileta pamoja wawakilishi kutoka mabara yote ya dunia, mashindano yaliyofanyika tarehe 25 mwezi Mei mwaka 1924 wakati wa michezo ya Olimpiki ya majira ya joto huko Paris Ufaransa.

Azimio namba A/RES/78/281 pamoja na mambo mengine linatambua mawanda ya mpira wa miguu duniani na athari zake Chanya katika nyanja mbali mbali ikiwemo biashara, amani na diplomasia na linatambua kuwa mpira wa miguu unajenga nafasi ya ushirikiano.

Nukuu za wachezaji nguli wa mpira wa miguu duniani

“Nimenufaika moja kwa moja na nguvu ya michezo katika kusongesha maisha yenye afya bora na nimejizatiti kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO kusambaza manufaa haya ya mpira wa miguu,” anasema Didier Drogba, Balozi mwema wa WHO.

Naye Marta Vieira da Silva, balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women anasema “mpira wa miguu unaunganisha dunia. Nataka kila mtoto wa kike awe na fursa ya kufikia ndoto ya kile anachotaka kuwa na awe na furaha.”