Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja kamili wa vita Sudan, jumuiya ya kimataifa inasemaje?

Picha iliyopigwa kutoka juu ikionesha watoto na familia zao wakiwa wamesimama karibu na makazi ya muda kwenye kituo cha Khamsa Dagiga kwa watu waliokimbia makazi yao katika Mji wa Zelingei, Darfur ya Kati, Sudan.
© UNICEF/Spalton
Picha iliyopigwa kutoka juu ikionesha watoto na familia zao wakiwa wamesimama karibu na makazi ya muda kwenye kituo cha Khamsa Dagiga kwa watu waliokimbia makazi yao katika Mji wa Zelingei, Darfur ya Kati, Sudan.

Mwaka mmoja kamili wa vita Sudan, jumuiya ya kimataifa inasemaje?

Amani na Usalama

Leo Aprili 15, 2024 ni mwaka mmoja kamili tangu vita ya sasa nchini Sudan ilipoanza kutokana na mvutano mkali kati ya pande mbili za wanajeshi wanaohasimiana (Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF na Vikosi vya jeshi la Sudan, SAF katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Katika kuuangazia mwaka huu mmoja tangu kuzuka kwa mzozo huo ambao umezua janga kubwa zaidi duniani wa watu kuyahama makazi yao, hii leo jijini Paris Ufaransa unafanyika Mkutano wa Kimataifa wa Misaada ya Kibinadamu kwa ajili ya Sudan na Majirani zake.

Aidha siku hii imetumiwa na viongozi wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kupaza sauti kuhusu mzozo huu wa kutisha wa Sudan.

António Guterres – Ni jinamizi

"Mwaka mmoja umepita tangu kuzuka kwa vita nchini Sudan, ambayo imeibua orodha ya mambo ya kutisha." Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko mjini Paris, Ufaransa kwa njia ya video amewaeleza waliohudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Misaada ya Kibinadamu kwa Sudan na Majirani zake, katika kuuangazia mwaka mmoja tangu kuzuka kwa mzozo huo ambao umezua janga kubwa zaidi duniani wa watu kuyahama makazi yao.

Jinamizi la umwagaji damu ambalo limeua zaidi ya watu 14,000 na kujeruhi wengine 33,000. Jinamizi la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana. Jinamizi la uharibifu ambalo limepunguza makazi, hospitali, shule na miundombinu mingine muhimu kuwa kifusi. Jinamizi la njaa na kuhama makazi, huku zaidi ya watu milioni nane wakikimbia makazi yao. Na jinamizi kwa majirani wa Sudan, ambao wanazidi kuhisi athari za mzozo huu mbaya.

Tunahimiza juhudi za upatanishi za kimataifa zinazofaa na zilizoratibiwa kukomesha mapigano. Na tunatoa wito kwa makundi ya kiraia  ikiwa ni pamoja na wale wanaowakilisha wanawake na vijana kusaidia kuongoza mchakato wa kisiasa unaojumuisha ili kurejesha mabadiliko ya kidemokrasia ya Sudan.

“Naahidi uuungaji mkono ulio kamilifu kutoka kwa Umoja wa Mataifa.”

Volker Türk – Raia wanapewa silaha

Mzozo wa mwaka mzima nchini Sudan tayari umesababisha mateso na vifo vingi lakini hali inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na habari kwamba pande zinazozozana zinawapa raia silaha, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ameeleza.

Mwaka mmoja tangu siku ya kwanza mapigano makali yalipozuka kati ya wanajeshi hasimu wa Sudan, Volker Türk alionya kuhusu kuongezeka kwa uhasama na mapigano.

"Watu wa Sudan wamekumbwa na mateso yasiyoelezeka wakati wa mzozo ambao umekuwa na mashambulizi ya kiholela katika maeneo yenye wakazi wengi, mashambulizi ya kikabila, na matukio makubwa ya unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro. Watoto kuhusishwa jeshini na kutumiwa katika mzozo pia kunatia wasiwasi sana.” Anaeleza Bwana Türk.

Pia Türk amesisitiza uwezekano wa umwagaji damu zaidi, wakati makundi matatu yenye silaha yalitangaza kwamba wanajiunga na Jeshi la Sudan katika vita yao dhidi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka na " kuwapa raia silaha”.

Tangu mapigano yalipozuka tarehe 15 Aprili 2023, zaidi ya watu milioni nane wamekimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na watu takribani milioni mbili kwenda nchi jirani.

"Takriban watu milioni 18 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, milioni 14 kati yao wakiwa watoto, na zaidi ya asilimia 70 ya hospitali hazifanyi kazi tena huku kukiwa na ongezeko la magonjwa ya kuambukiza. Hali hii mbaya lazima isiruhusiwe kuendelea." Kamishna Mkuu Türk aamesisitiza mkutanoni mjini Paris.

UNICEF - Utapiamlo

Likirejea wasiwasi huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kuwa watoto wapatao milioni 8.9 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula; hii inajumuisha milioni 4.9 katika viwango vya dharura.

"Takriban watoto milioni nne walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kukabiliwa na utapiamlo uliokithiri mwaka huu", wakiwemo 730,000 kutokana na utapiamlo unaotishia maisha, UNICEF imefafanua katika taarifa waliyoitoa Jumapili yarehe 14 Aprili.

"Karibu nusu ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali wako katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa na ambako kuna mapigano yanayoendelea.” Anabainisha Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Ted Chaiban.

Education Cannot Wait – Elimu Haiwezi Kusubiri

Na katika onyo kwamba nchi nzima inaweza kukumbwa na mapigano ambayo yamesababisha nusu ya watu wa Sudan kuhitaji misaada ya kibinadamu, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuchagiza elimu kwenye maeneo ya mizozo, Education Cannot Wait, ECW, au Elimu Haiwezi Kusubiri, unasisitiza kuwa watu wanne kati ya milioni nane waliofurushwa na ghasia hizo ni watoto.

Mgogoro huo "unaendelea kuchukua maisha ya watu wasio na hatia, huku zaidi ya watoto 14,000, wanawake na wanaume wakiripotiwa kuuawa." Anasema Yasmine Sherif, Mkurugenzi Mtendaji wa Education Cannot Wait.

Bi. Sherif anarudia kueleza wasiwasi mkubwa kwamba Sudan sasa ina mojawapo ya matatizo mabaya zaidi ya elimu duniani, huku zaidi ya asilimia 90 ya watoto milioni 19 wenye umri wa kwenda shule nchini humo wakishindwa kupata elimu rasmi.

Shule nyingi zimefungwa au zinatatizika kufunguliwa tena nchini kote, na kuwaacha karibu watoto milioni 19 wenye umri wa kwenda shule katika hatari ya kupoteza masomo yao.

Hadi sasa, mfuko huo wa kimataifa umetoa karibu dola milioni 40 kusaidia elimu kwa waathirika wa mgogoro nchini Sudan na kwingineko, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.

"Bila ya hatua za haraka za kimataifa, janga hili linaweza kuikumba nchi nzima na kuwa na athari mbaya zaidi kwa nchi jirani, wakati wakimbizi wanakimbia kuvuka mipaka na kuingia Mataifa Jirani." Anaonya Bi. Sherif.

UN Women - Mwaka wa mateso kwa wanawake na wasichana

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women linasisitiza kwamba hatua za haraka lazima zichukuliwe ili kuhakikisha ulinzi wa wanawake na wasichana, kusaidia uwezeshaji wao kiuchumi, na kuwajumuisha katika mazungumzo ya amani na kufanya maamuzi. Tunawahimiza wadau wa kimataifa na wafadhili kuwekeza katika mashiŕika ya ndani, yanayoongozwa na wanawake na kuweka vipaumbele vya ŕasilimali ili kushughulikia vipimo vya kijinsia vya mzozo huu.

Wanawake na wasichana wa Sudan wanalipa gharama kubwa kwa ghasia hizi, wakibeba mzigo mkubwa wa janga la kibinadamu ambalo bado halionekani kwa ulimwengu. Sudan ni miongoni mwa matatizo makubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani. Asilimia 53 ya wakimbizi wa ndani ni wanawake na wasichana, na kuna hatari kubwa kwamba ghasia hizo hivi karibuni zitasababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani. Zaidi ya akina mama wachanga 7,000 wanaweza kufariki katika miezi ijayo ikiwa mahitaji yao ya lishe na afya yatabaki kutotimizwa.

UN Women inathibitisha kwamba zaidi ya watu milioni 6.7 wako katika hatari ya unyanyasaji wa kijinsia, na ripoti za unyanyasaji unaotekelezwa na wapenzi wa karibu, unyanyasaji na unyonyaji wa kingono, na usafirishaji haramu wa watu vimeenea na kuongezeka. Walionusurika huripoti mara chache kuweza kupata huduma au kuripoti kwa mamlaka. Athari za kiuchumi za mzozo huo zimewaweka pembeni zaidi wanawake, kuwanyima fursa za kujikimu na kuwasukuma wengi kuelekea hatua kali na hatari ya unyonyaji na unyanyasaji wa kijinsia wanapotafuta kusaidia familia zao.

IOM – Tafadhali tafuta amani

Mjini Paris leo, mkutano wa kibinadamu unaipa jumuiya ya kimataifa fursa ya kuanza kurekebisha hali hii, ili kurejesha ahadi ya ubinadamu. Mashirika ya misaada, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM yatawasilisha kesi taarifa zao kwa serikali za wafadhili, na kuwaomba kusaidia kupunguza moja ya machafuko mabaya zaidi ya kibinadamu kuwahi kuona na ulimwengu katika kumbukumbu za hivi karibuni.

 "Zaidi ya ufadhili, tunachohitaji zaidi ya yote, kama tunavyohitaji katika sehemu nyingine nyingi za dunia, ni amani. Sisi sote katika jumuiya ya kibinadamu tunaomba hili kwa kila kiongozi, kwa yeyote anayeweza kushawishi pande zinazopigana: watu wanateseka, maisha yao yako ukingoni. Tafadhali tafuta amani.”