Kura mbili za turufu zaipinga rasimu ya azimio la Marekani la “umuhimu mkubwa” kusitisha mapigano Gaza
Kura mbili za turufu zaipinga rasimu ya azimio la Marekani la “umuhimu mkubwa” kusitisha mapigano Gaza
Katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokaa asubuhi hii ya Machi 22 saa za New York Marekani, Urusi na China zimepinga kwa kura ya turufu rasimu ya azimio la Marekani lililotaka "ulazima" kwa usitishaji mapigano haraka na thabiti "kuwalinda raia kutoka pande zote," kuwezesha uwasilishaji wa misaada inayohitajika na kuunga mkono mazungumzo yanayoendelea kati ya Israeli na Hamas.
Pendekezo lililowasilishwa na Marekani kwa Baraza la Usalama limesema kwamba usitishaji vita huko Gaza, utoaji wa misaada na uungaji mkono kwa mazungumzo ni "muhimu sana"; lakini wakosoaji wanaonesha kuwa lilikuwa linakosa kusema hitaji la wazi la kusitisha mapigano; pendekezo mbadala linatayarishwa na wajumbe 10 waliochaguliwa wa Baraza la Usalama.
Algeria pia imepiga kura ya kupinga (sio ya turufu kwa kuwa Algeria sio mwanachama wa kudumu wa Baraza), wakati Guyana haikupiga kura na nchi 11 zilizosalia zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo.
Pendekezo hilo lilisema kuwa ni "muhimu sana" kuwa na "sitisho la mapigano mara moja na endelevu ili kulinda raia kutoka pande zote," kuwezesha uwasilishaji wa misaada "muhimu", na kuunga mkono mazungumzo yanayoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas kuelekea kukomesha ghasia endelevu, zinazohusishwa kuachiliwa kwa mateka wote.
Mabadiliko ya msimamo wa Marekani
Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo kati ya wajumbe wa Baraza la Usalama, rasimu ya Marekani inaashiria mabadiliko ya msimamo ikilinganishwa na mara ya mwisho wajumbe walikutana, Februari 20, wakati diplomasia ya Marekani ilipopiga kura ya turufu kwa azimio la Algeria kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja.
Hati hiyo pia inadai ufikiaji wa kibinadamu kwa mateka, ulinzi wa raia na ujenzi mpya unaoongozwa na Umoja wa Mataifa. Inalaani vitendo vya ugaidi, inataka kuheshimiwa kwa mikataba ya kibinadamu na inasisitiza kuunga mkono suluhu ya Serikali mbili.
Akifungua mkutano huo kwa kuelezea pendekezo hilo, Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield amesema kuwa Marekani inataka usitishaji vita wa haraka na wa kudumu. Hata hivyo, amesema kwamba ni muhimu kufanya "kazi ngumu ya diplomasia" ili kufanya lengo hili kuwa kweli na hii inapaswa kuwa "halisi kwenye eneo husika".
Kwake, azimio hilo lingesaidia kuishinikiza Hamas kukubaliana na makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka. Amesema kuwa azimio hilo hatimaye lingelaani Hamas, lakini pia kupunguza mateso na ghasia zinazoikumba Gaza. Balozi wa Marekani pia amesisitiza kwamba uvamizi wa Rafah ungekuwa kosa.
Upinzani wa Urusi
Kabla ya kupiga kura dhidi ya azimio hilo, Balozi wa Urusi, Vassily Nebenzia, amesema Marekani imeahidi mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mwakilishi huyo wa Urusi anadai kuwa Marekani imetambua hitaji la kusitisha mapigano wakati ambapo "zaidi ya watu elfu 30 wa Gaza wamekufa". Kwa mwanadiplomasia huyo, Marekani ilikuwa inajaribu "kuuza bidhaa" kwa Baraza kwa kutumia neno ‘imperative’ / “muhimu” katika azimio lake. Kulingana naye, "hii haitoshi" na Baraza lazima "lidai kusitishwa kwa mapigano".
Vassily Nebenzia amesema hakuna wito wa kusitisha mapigano katika azimio hilo, akishutumu uongozi wa Marekani kwa "kudanganya kimakusudi jumuiya ya kimataifa." Amesema pendekezo hilo ni "kucheza na wapiga kura wa Marekani."