Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuunganishwa kidigitali sio fursa bali haki ya kimsingi

Carine. mhandisi wa programu za kompyuta akiwa nyumbani kwao Kigali nchini Rwanda akitumia kishkwambi kukamilsha programu yake iitwayo Save and Save.
© UNICEF/Mary Gelman
Carine. mhandisi wa programu za kompyuta akiwa nyumbani kwao Kigali nchini Rwanda akitumia kishkwambi kukamilsha programu yake iitwayo Save and Save.

Kuunganishwa kidigitali sio fursa bali haki ya kimsingi

Utamaduni na Elimu

Wakati dunia ikiwa na maono mbalimbali juu ya ukuaji wa mtandao na namna unavyoweza kuwasaidia, Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda Ozzonia Ojielo amesema ni vyema maono hayo yakamjumuisha kila mwananchi.

Akizungumza katika jukwaa la kujadili utawala wa mtandao lililofanyika Kigali nchini Rwanda likikutanisha wadau wa masuala ya mtandao waliokutana kuangalia namna bora ya kuhakikisha jamii nzima inanufaika na maendeleo ya kiteknolojia yanayoletwa na huduma ya mtandao Ojielo amesema “Ahadi yetu ya kumjumuisha kila mtu inaanza kwa kuhakikisha kuna upatikanaji sawa wa mtandao kote nchini Rwanda kuanzia mijini mpaka vijijini. Kuunganishwa na mtandao haipaswi kuwa fursa bali haki ya msingi inayopatikana kwa wote.” 

Mkuu huyo wa UN nchini Rwanda amesema pamoja na kufikishiwa huduma ya mtandao lakini pia wananchi wapatiwe elimu. “Kwa kukuza elimu ya kidigitali, tutawawezesha watu binafsi kuchangamkia fursa katika elimu, ujasiriamali, na ushiriki wa kiraia, hatimaye hivi vyote vitasaidia kuendeleza maendeleo ya taifa letu.” 

Katika hotuba yake hiyo pia ameipongeza serikali ya Rwanda kwa kupitisha sheria ya kulinda taarifa za watumia mitandao ya mwaka 2021 pamoja na sera ya kitaifa ya Akili Mnemba au AI ya mwaka 2022 na kusema juhudi hizo zinaonesha nia ya dhati ya serikali ya Rwanda ya kuendelea kidijitali, kibunifu na kuwalinda wananchi wake.