Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasubiri kibali cha kupitisha vifaa vya matibabu Rafah kuelekea Gaza

Lori jekundu la mizigo lililojaa vifaa vya afya vya Shirika la Afya Duniani katika uwanja wa ndege wa Al-Arish nchini Misri, likiwa njiani kuelekea Gaza.
WHO Vifaa vya matibabu kwa ajili ya Gaza vimesafirishwa kutoka bohari ya WHO huko Dubai, Falme za kiarabu na hivi sasa viko mpakani mwa Misri na Israel vikisubiri kibali cha kuingizwa Gaza kupitia kivuko cha Rafah

WHO yasubiri kibali cha kupitisha vifaa vya matibabu Rafah kuelekea Gaza

Afya

Ndege iliyobeba shehena ya mita za ujazo 78 za vifaa muhimu vya matibabu imetua Cairo nchini Misri tayari kupelekwa Ukanda wa Gaza huko Mashariki ya Kati ambako mapigano kati ya wanamgambo wa Hamas na jeshi la Israel yameongeza mahitaij ya huduma za afya kwa maelfu ya majeruhi.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya WHO Kanda ya Mashariki mwa Mediteranea iliyotolewa leo huko Cairo, Misri inasema kinachosubiriwa sasa ni kufunguliwa kwa kivuko cha njia ya Rafah itakayotumika kupitishia dawa na vifaa hivyo vya kibinadamu.

Saa zinayoyoma, kibali cha kufunguliwa Rafah kikisubiriwa

WHO inasema kila saa inayopita vifaa hivyo vikiwa kwenye upande wa mpaka wa Misri, idadi ya wavulana, wasichana, wanawake, wanaume, watoto, wazee na wenye ulemavu wanaofariki dunia itaongezeka, wakati vifaa hivyo viko kilometa zisizozidi 20.

Vifaa ni pamoja na dawa za kutibu kiwewe, na dawa za kutibu majeruhi 1200, pamoja wagonjwa 1500 wa moyo, kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya njia ya hewa.

Halikadhalika shehena inajumuisha vifaa vya matibabu kwa ajili ya watu 300,000 wakiwemo wajawazito.

WHO inasema itashirikiana na mashirika ya Hilal Nyekudu ya Misri na Palestina kuhakikisha usafirishaji na usambazaji salama wa vifaa hivyo Gaza kupitia Misri.

Misri imekubali Rafah itumike, Israeli bado imefunga

Tarehe 9 mwezi huu wa Oktoba, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alikutana na Rais Abdel Fattah El-sisi wa Misri ambaye alikubali ombi la WHO la kufanikisha upelekaji wa vifaa ya matibabu na kiutu kwenda Gaza kupitia njia ya Rafah.

Ingawa upande wa Misri wa kivuko hicho unapitika, upande wa Israeli bado umefungwa.