Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka tano- UNEP

Nyundo ya mahakamani
UNODC
Nyundo ya mahakamani

Kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka tano- UNEP

Tabianchi na mazingira

Idadi ya kesi zinazofikishwa mahakama duniani kote kuhusu mabadiliko ya tabianchi imeongezeka maradufu tangu mwaka wa 2017, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria cha Mabadiliko ya Tabianchi cha Sabin katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Taarifa iliyotolewa leo na UNEP huko jijini Nairobi Kenya inaonesha kuwa kesi hizo zinaanza kuwa nguzo muhimu ya kupelekea kushughulikia mazingira na kuyapatia haki ikinukuu Ripoti ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Duniani: Uchanganuzi wa Mwaka wa 2023. 

Mifano ya kesi zilizofunguliwa mahakamani 

Miongoni mwa kesi hizo ni ile ya nchini Uholanzi ambako mahakama nchini  humo iliamrisha kampuni ya mafuta na gesi ya Shell kutii Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wake wa hewa ya ukaa kwa asilimia 45 kutoka kwa viwango vya mwaka wa 2019 kufikia mwaka wa 2030.  

Nchini Australia, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema kwa mara ya kwanza kwamba nchi hiyo imekiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu kupitia kutoweka sera na kutochukua hatua za kushughulikia mazingira, na hivyo serikali ilikiuka wajibu wake wa haki za binadamu kwa wakazi wa visiwa vya Torres Strait. 

Ripoti hii inatokana na uchanganuzi wa kesi zinazojikita kwa sheria, sera na sayansi ya mabadiliko ya tabianchii kufikia tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2022 na  Kanzidata ya Kituo cha Sheria cha Mabadiliko ya Tabianchi cha Sabin nchini Marekani na Kanzidata ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Ulimwenguni.  

Watu wanageukia mahakama kusaka haki zao  

"Sera za mazingira zingali nyuma sana  kwa kuzingatia kile kinachohitajika ili kudhibiti viwango vya joto duniani visizidi nyuzijoto 1.5, katika kipimo cha selsiyasi huku matukio mabaya ya hali ya hewa na joto kali vikichemsha sayari yetu," amesema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. 

Amesema ”watu wanazidi kugeukia mahakama ili kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi, ili kuwajibisha serikali na sekta binafsi na kufanya kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa nguzo muhimu ya kushughulikia mazingira na kukuza haki ya mazingira." 

Idadi jumla ya kesi za mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka zaidi ya maradufu tangu toleo la kwanza kwa kuongezeka kutoka 884 katika mwaka wa 2017 hadi 2,180 katika mwaka wa 2022.  

Marekani inaongoza kwa kesi, kesi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinakita mizizi kote duniani, huku takriban asilimia 17 ya kesi zikiripotiwa katika nchi zinazoendelea, zikiwemo Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo (SIDS). 

Ripoti hiyo imezinduliwa siku moja kabla ya maadhimisho ya kwanza ya tamko la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu upatikanaji wa mazingira safi na bora kama haki ya binadamu wote. 

Soma ripoto kwa kina hapa.