Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN waitaka Libya kuondoa sera inayowataka wanawake na wasichana kusafiri na Mahram

Uwanja katika jengo la kati huko Tripoli, mji mkuu wa Libya.
© UN Photo/Abel Kavangh
Uwanja katika jengo la kati huko Tripoli, mji mkuu wa Libya.

UN waitaka Libya kuondoa sera inayowataka wanawake na wasichana kusafiri na Mahram

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa hii leo wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu sera ya kibaguzi iliyotolewa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya (GNU) mwezi Aprili 2023 ambayo inazuia haki za wanawake na wasichana kusafiri nje ya nchi bila mlezi wa kiume au Mahram.

Taarifa ya wataalamu hao iliyotolewa leo na Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR kutoka Geneva Uswisi imesema sera hiyo “Siyo tu ni yakibaguzi, lakini pia inazuia uhuru wa wanawake na wasichana kutoka sehemu moja Kwenda nyingine ikiwemo wanafunzi wanaenda masomoni nje ya nchi.” 

Tayari sera hiyo imekwishaanza kufanya kazi na wale wasio na Mahram wamekuwa wakinyimwa vibali.

Sera hiyo mpya imeripotiwa kuanza kutekelezwa bila tangazo lolote rasmi au la awali na imewataka wanawake na wasichana wote wanaosafiri kujaza fomu ambayo inawakata kutoa taarifa za kibinafsi, sababu za kusafiri bila mlezi wa kiume au Mahram, na maelezo ya historia yao ya awali ya kusafiri bila Mahram.

“Wanawake na wasichana wanaokataa kujaza au kuwasilisha fomu hiyo wameeleza kukataliwa kuondoka. Kizuizi hicho kinaashiria mmomonyoko zaidi wa haki za wanawake na wasichana nchini Libya na unatoa ishara mbaya,” wamesema wataalam hao na kukumbusha kuwa “Usawa na utu wa wanawake lazima uhakikishwe.”

Wataalamu hao wameeleza kuwa wanawasiwasi na ripoti za majaribio ya Shirika la Usalama wa Ndani la Libya (ISA) kuwatisha watetezi wa haki za binadamu, wakiwemo wanawake, ambao wamekuwa wakipaza sauti zao kuzungumzia dhidi ya sera hizi.

Wamezitaka mamlaka hizo kuondoa hitaji hili la kibaguzi na kuzuia vitisho, unyanyasaji na mashambulizi yote dhidi ya wanawake na watetezi wa haki za binadamu ambao wamepinga sera hii ya kibaguzi.

Wameikumbusha Libya kutekeleza wajibu wake wa Kimataifa na kitaifa wa mtu yeyote kutibaguliwa na uwepo wa usawa na haki ya faragha. 

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa waliotoa taarifa hii ni Reem Alsalem, ambaye ni Ripota Maalum kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, sababu na matokeo yake; Mary Lawlor, Ripota Maalum kuhusu hali ya watetezi wa haki za binadamu; Dorothy Estrada-Tanck (Mwenyekiti), Ivana Radačić (Makamu Mwenyekiti), Elizabeth Broderick, Meskerem Geset Techane na Melissa Upreti, Kikundi Kazi kuhusu ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana; Ana Brian Nougrères, Mwandishi Maalum kuhusu haki ya faragha; Farida Shaheed, Ripota Maalum kuhusu haki ya kupata elimu.

Kufahamu kazi zinazofanywa na wataalamu hawa wa umoja wa Mataifa bofya hapa.