Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa walaani mwanaharakati kufungwa nchini Misri

Maisha ya kila siku katika moja ya mitaa ya Cairo, mji mkuu wa Misri.
Unsplash/Simon Berger
Maisha ya kila siku katika moja ya mitaa ya Cairo, mji mkuu wa Misri.

Umoja wa Mataifa walaani mwanaharakati kufungwa nchini Misri

Haki za binadamu

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesikitishwa na hukumu iliyotolewa jana tarehe 18 Julai 2023 nchini Misri dhidi mtafiti na mtetezi wa haki za binadamu Patrick George Zaki aliyehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa sababu ya kutoa maoni yake.


 

Msemaji wa Ofisi hiyo ya Haki za Binadamu Seif Magango akiwa mjini Geneva Uswisi amesema “tunahimiza kuachiliwa kwake huru mara moja na bila masharti.”

Magango amesema wana wasiwasi takriban miaka miwili baada ya kuondolewa kwa hali ya tahadhari nchini Misri bado mahakama za dharura zinaendelea kutoa hukumu dhidi ya watu binafsi, ikiwa ni pamoja na wale wanaotekeleza haki zao za kibinadamu katika tarehe ambazo hali ya tahadhari ilikwisha ondolewa.

“Sambamba na kuendelea kwa matumizi ya sheria yenye vikwazo, tabia hii inaleta athari mbaya miongoni mwa watendaji wa mashirika ya kiraia na kupunguza nafasi ya kiraia nchini, licha ya mchakato unaoendelea wa mazungumzo ya Kitaifa," amesisitiza msemaji huyo.

Mwanaharakati Zaki alikamatwa mwezi Februari mwaka 2020 alipokuwa ziarani nyumbani akitokea masomoni nje ya nchi na akashitakiwa kwa “kueneza habari za uongo kuhusu hali ya ndani ya nchi” katika makala aliyoichapisha kuhusu jamii yake ya Coptic, ambayo ni jamii ndogo huko nchini Misri.

Ofisi ya Haki za binadamu imesema Zaki aliwekwa kizuizini kabla ya kufunguliwa mashtaka kwa takriban miaka miwili na inasemekana aliteswa, ikiwa ni pamoja na kupigwa na shoti ya umeme.