Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu laombwa kuchukua hatua kuhusu wakimbizi wa ndani

Watoto wakiteka maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Rusayo, DRC.
George Musubao
Watoto wakiteka maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Rusayo, DRC.

Baraza la haki za binadamu laombwa kuchukua hatua kuhusu wakimbizi wa ndani

Wahamiaji na Wakimbizi

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi wa ndani Paula Gaviria ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa idadi ya wakimbizi wa ndani inazidi kufurutu ada na huo ni ukweli wa kutisha. 

Akizungumza katika Baraza hilo jijini Geneva Uswisi Gaviria amesema takwimu za mwaka jana 2022 duniani kote zinaonesha kuongezeka kwa kiwango kisicho kifani ambapo watu milioni 71 walilazimika kuyakimbia makazi yao na kuliomba Baraza hilo kulichukulia suala hili kwa umuhimu mkubwa wakijikita mbali zaidi ya takwimu. 

"Idadi pekee haziwezi kujumuisha ukubwa, upana, utata, na mateso makubwa ya binadamu yanayokabiliwa na watu waliokimbia makazi yao," alisema Mtaalamu huyo wa haki za binadamu za wakimbizi wa ndani.

"Nyuma ya idadi hiyo kuna maisha na historia za kila mtu kibinafsi ambao wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao na kunusurika ukiukwaji wa haki za binadamu na dhuluma zisizofikirika," alisema wkati akisoma ripoti yake ya kwanza kwa Baraza la Haki za Kibinadamu.

Mtaalamu huyo ametaka hatua zichukuliwe za kushughulikia suala hilo kwani watu wengi zaidi kuliko hapo awali wanalazimika kutoroka ndani ya nchi zao wenyewe, wakifukuzwa kutoka makwao kutokana na migogoro, ghasia, maafa, athari za mabadiliko ya tabianchi na ukiukwaji wa haki za binadamu.