Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dhima ya teknolojia katika Ugaidi kutathminiwa nchini India kuanziaIjumaa

Balozi Ruchira Kamboj, Mwakilishi wa kudumu wa India kwenye UN, na Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Usalama la UN ya kukabili ugaidi
UN /Eskinder Debebe
Balozi Ruchira Kamboj, Mwakilishi wa kudumu wa India kwenye UN, na Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Usalama la UN ya kukabili ugaidi

Dhima ya teknolojia katika Ugaidi kutathminiwa nchini India kuanziaIjumaa

Amani na Usalama

Kesho kutwa Ijumaa huko nchini India, Kamati ya kukabili ugaidi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itakutana nchini India kutathmini vitisho vipya duniani vitokanavyo na teknolojia mpya.

Mkutano huo wa siku mbili ni wa kwanza kufanyika nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani tangu mwaka 2015.

Mjadala utajikita kwenye maeneo matatu makuu: Intaneti na mitandao ya kijamii; Ufadhili wa mitandao ya kigaidi duniani na kuenea kwa matumizi ya mifumo ya angani isiyo na rubani kama vile droni.

Teknolojia hizo mpya zinakua kwa kasi kubwa na zinatumika mara kwa mara katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo kwenye usalama wa taifa na kukabili ugaidi.

Hata hivyo teknolojia hizo zinatumiwa vibaya na vikundi vya kigaidi kwa manufaa yao binafsi yasio na nia njema.

Ndege zisizo na rubani au droni zina uwezo wa hali ya juu wa ufuatiliaji wa mambo kutoka angani
© Unsplash/Peter Fogden
Ndege zisizo na rubani au droni zina uwezo wa hali ya juu wa ufuatiliaji wa mambo kutoka angani

Teknolojia mpya kwa ugaidi?

Kwa sasa India ndio inashikilia kiti cha Uenyekiti wa Kamati hiyo hadi mwishoni mwa mwaka huu ambao akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Mwakilishi wa Kudumu wa India Kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ruchira Kamboj ambaye ndiye Mwenyekiti amesema, kikao hicho kitatathmini maendeleo ya hivi karibuni na ushahidi utokanao na tafiti ya uhusiano kati ya ugaidi na matumizi ya teknolojia.

Amesema “mkutano utaleta pamoja ufahamu wa kutosha na utaalamu wa kisasa kuhusu hoja ya ugaidi na washiriki ni nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wadau wanaotumia teknolojia hizo na wadau wengine wakuu.”

Mkutano pia utakuwa ni jukwaa la kubadilishana mawazo ya jinsi teknolojia inaweza kusaidia kukabili kusambaa kwa maudhui ya kigaidi mtandaoni na kukabili pia simulizi za kigaidi.

Halikadhalika washiriki wanatarajiwa kujadili jinsi magaidi wenye ujuzi wa kiteknolojia wanatumia ugunduzi wa kiteknolojia kusambaza fedha, kuuza bidhaa zao na kuomba misaada kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Nigeel kutoka Kenya anaongelea jinsi alikua bila baba yake ambaye aliuawa katika shambulio la Ubalozi wa Marekani mnamo 1998 iliathiri maisha yake.
UNCCT
Nigeel kutoka Kenya anaongelea jinsi alikua bila baba yake ambaye aliuawa katika shambulio la Ubalozi wa Marekani mnamo 1998 iliathiri maisha yake.

Ndege zisizo na rubani na akili bandia

Hofu nyingine iliyoko na itakayomulikwa ni matumizi kwa nia mbaya ya uchapishaji wa chapa tatu au 3D, maroboti, akili bandia na mifumo ya angani isiyo na usimamizi.

Kuhusu ongezeko la matumizi ya droni au ndege zisizo na rubani, Mratibu wa Habari na Teknolojia wa Kamati hiyo, Jennifer Bramlette amesema tayari wajumbe wamechukua hatua kushughulikia suala hilo.

“Bilas haka, hakuna maeneo ya zuio la kuruka ndege kwenye maeneo ya viwanja vya ndege au miundombinu muhimu. Bilas haka, kampuni zenyewe zimechukua hatua kujenga mifumo ya udhibiti wa kijiografia ili iwapo droni inabainika kuruka katika maeneo fulani, inaweza kushushwa angani.”

Amesema kuna mijadala kadhaa inaendelea jinsi gani droni zinauzwa na nani anaweza kununua.

Makubaliano ya mwisho

Kutokana na ugumu wa suala zima, na kasi ya mapinduzi yake, matarajio ni kwamba wajumbe watakuwa na nyaraka ya mwisho ambayo itatoa mwelekeo wa jinsi magaidi wanatumia teknolojia, kwa lengo la kufunga simulizi zao na matumizi ya teknolojia.

Kuhusu Kamati

Kamati ya kukabili ugaidi ya Baraza la Usalama la UN iliundwa kwa kauli moja tarehe 28 mwezi Septemba mwaka 2001, kufuatia shambulio la kigaidi dhidi ya Marekani tarehe 11 Septemba 2001 na wanachama ni wajumbe wote 15 wa Baraza la Usalama.