Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guinea ya Ikweta yaungana na Uganda, Togo, Benin na Côte d'Ivoire waliotokomeza Malale hivi karibuni

Kung'atwa na mbung'o husababisha ugonjwa wa malale kwa binadamu.
Geoffrey M. Attardo, Mtafiti, Yale School of Public Health
Kung'atwa na mbung'o husababisha ugonjwa wa malale kwa binadamu.

Guinea ya Ikweta yaungana na Uganda, Togo, Benin na Côte d'Ivoire waliotokomeza Malale hivi karibuni

Afya

Juhudi za kutokomeza ugonjwa wa Malale au human African trypanosomiasis (HAT), zinaendelea kuonesha maendeleo bora, kulingana na malengo yaliyowekwa katika mpango wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, ya mwaka 2030 ya kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa. 

 

Guinea ya Ikweta sasa imethibitishwa na WHO kuwa nchi ya hivi punde zaidi kutokomeza aina ya gambiense ya ugonjwa huo wa malale kama tatizo la afya ya umma ndani ya mipaka yake. 

Malale ina aina mbili kuu zinazojulikana kama gambiense na rhodesiense, na kwa ujumla huambukizwa kwa kung’atwa na aina ya nzi walioambukizwa. 

“Maambukizi ya jumla ya malale aina ya Gambinse yamepungua kwa kasi karne hii.” WHO inaeleza ikifafanua kwamba mnamo mwaka 2021, ripoti za maambukizi kwa watu 750 ziliripotiwa katika nchi 11 zenye ugonjwa huo hii iliwakilisha punguzo la asilimia 95 la idadi ya maambuki ikilinganishwa na takwimu ya mwaka 2001 ya mambukizi 26,095. “Guinea ya Ikweta sasa inaungana na Benin, Côte d'Ivoire, Togo na Uganda kwenye orodha ya nchi zilizotangazwa na WHO kuondokana na malale.” 

Kazi ya muda mrefu na kujitolea kwa Wizara ya Afya ya Guinea ya Ikweta, kupitia Mpango wake wa Kitaifa wa Kudhibiti Malale (PNCTHA), imeruhusu nchi kufikia kiwango kilichowekwa ili kuhalalisha kutangazwa kuwa imeutokomeza ugonjwa huo. 

Kiwango hiki kinafafanuliwa kuwa chini ya kisa kiomja cha maambukizi kwa kila wakazi 10,000 kwa wastani, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, katika ‘wilaya zote za afya nchini’.

Uthibitishaji wa utokomezaji unahitaji nchi kuwasilisha ripoti nyingi za kutosha kwa WHO. Ripoti hizo hutathminiwa na kundi huru la wataalam, ambao huamua ikiwa vigezo vya kuondolewa kama tatizo la afya ya umma vimefikiwa. 

Mnamo tarehe 10 Juni 2022, mwakilishi wa WHO katika Guinea ya Ikweta, Dkt. George Fom Ameh, alituma barua rasmi ya kukiri mafanikio haya kwa Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Dkt. Diosdado Vicente Nsue Milang. Barua hiyo ilitiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus 

WHO kupitia taarifa iliyoichapisha leo Juni, 20, 2022, imesema, kutokomezwa Malale aina ya Gambinse kama tatizo la afya ya umma ni hatua muhimu katika kufikia lengo kubwa zaidi la kukomesha maambukizi.

Guinea ya Ikweta sasa imejitolea kudumisha uwezo wake wa ufuatiliaji, ili kuhakikisha kuwa uchunguzi na utambuzi unaendelea katika watu walio katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. Inasalia kujitolea pia kuhakikisha kuwa kuna matibabu ya kutosha kwa visa vyovyote vipya vinavyogunduliwa, na kudhibiti idadi ya nzi wa maambukizi.