Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda nayo yaanza kutoa chanjo dhidi ya COVID-19

Mfanyakazi wa afya nchini Uganda Dkt. Ombeva Malande akionesha kadi yake ya chanjo baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19 katika hospitali ya Mulago jijini Kampala.
WHO Uganda
Mfanyakazi wa afya nchini Uganda Dkt. Ombeva Malande akionesha kadi yake ya chanjo baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19 katika hospitali ya Mulago jijini Kampala.

Uganda nayo yaanza kutoa chanjo dhidi ya COVID-19

Afya

Nchini Uganda kazi ya kuwapatia chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 wafanyakazi walio mstari wa mbele wakiwemo wahudumu wa afya imeanza kufuatia taifa hilo la Afrika Mashariki kupokea shehena ya chanjo kutoka COVAX ambao ni mfumo wa kimataifa wa kusaka na kusambaza chanjo za COVID-19.

Kazi ya kutoa chanjo imefanyika katika hospitali ya Mulago iliyoko Kampala mji mkuu wa Uganda, ambapo miongoni mwa watu wa kwanza kupatiwa chanjo hiyo ni Waziri wa Afya Dkt. Jane Ruth Ocero.

Chanjo hii ya AstraZeneca ni sehemu ya dozi 864,000 zilizowasili Uganda tarehe 5 mwezi huu wa Machi kwa uratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

UNICEF inahusika na upatikanaji na uwasilishaji wa chanjo hizo pamoja na vifaa vingine husika kama vile mabomba ya sindano na visanduku vya kutupa sindano zilizotumika.

Catherine Ntabadde, ni mtaalamu wa mawasiliano UNICEF Uganda na anasema,"Nina furaha kufahamu kuwa wafanyakazi wetu wa afya ni miongoni mwa makundi ya kwanza kupatiwa chanjo hii, kwa sababu pindi wahudumu wa afya wanakuwa salama, tuna uhakika kuwa taifa liko salama kwa sababu tunataka kuona sekta ya afya inarejea katika utendaji wake kikamilifu. Pindi wafanyakazi wa afya wanapopata chanjo, wataweza kushughulikia mambo mengine. Na tunatumai kuwa hatimaye tutaweza kupunguza vifo vitokanavyo na COVID-19."

COVAX imetenga dozi milioni 3.5 za AstraZeneca kwa ajili ya Uganda kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu wa 2021. Dozi zilizosalia zaidi ya milioni 2.6 zinatarajiwa kufika Uganda mwezi Juni mwaka huu.

Wanaopatiwa chanjo kwa sasa pamoja na wahudumu wa afya ni watu wa usalama, walimu, watoa misaada na wale wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wenye magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, figo watapatiwa chanjo kadri zitakavyowasili nchini.

Nchi nyingine za Afrika ambazo tayari zimepokea chanjo dhidi ya Corona ni kupitia COVAX ni pamoja na Rwanda, Kenya, Ghana, na Cote D’Ivoire.