Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaya masikini Tanzania kunufaika na msaada wa dola milioni 3.74

Wakulima wadogo wanapokea msaada wa kuboresha usalama wa chakula baada ya kukumbana na athari za janga la COVID-19
IFAD/Joanne Levitan
Wakulima wadogo wanapokea msaada wa kuboresha usalama wa chakula baada ya kukumbana na athari za janga la COVID-19

Kaya masikini Tanzania kunufaika na msaada wa dola milioni 3.74

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP nchini Tanzania limepokea msaada wa dola milioni 3.74 kutoka serikali ya CANADA kwa ajili ya kusaidia miradi ya hifadhi za jamii kwa kaya masikini nchini humo. 

Akikabidhi msaada huo jijini Dar es Salaam, Balozi wa CANADA nchini Tanzania Pamela O’Donnell amesema ufadhili huo unalenga kuweka fedha mikononi mwa wanufaika ambao wengi wao wameathirika kiuchumi kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Canada inatambua hitaji la ulinzi wa jamii, kuwasaidia wanajamii walio katika mazingira magumu zaidi wakati wa shida. Mchango huu ni kielelezo cha kujitolea kwetu kuwa na mshikamano na kusimama Pamoja katika kufanya kazi Pamoja na washirika wa maendeleo katika kukabiliana na janga hili la ulimwengu ambalo halijawahi kutokea.” Amesema O’Donnell. 

Kwa upande wake mkurugenzi mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Sarah Gordon- Gibson akipokea msaada huo ameishukuru serikali ya Canada kwa kuunga mkono juhudi za kusaidia kaya masikini. 

“Msaada huu ni muhimu kwa kaya masikini kwakuwa utawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali kutokana na kuishi katika mazingira magumu, hasa wanawake na Watoto ambao wana jukumu kuu la usalama wa chakula na lishe. Fedha hizi zitawawezesha wanawake kupata chakula cha kutosha na kujikimu kwa mahitaji mengine muhimu ya familia zao.”

WFP inafanya kazi na serikali ya Tanzania kusaidia kaya masikini kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii, TASAF. 
Serikali ya Canada na WFP ni waumini wa msaada kwa kaya masikni kupitia utoaji fedha wa moja kwa moja kwa wanufaika.