Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Sigara ya  kielektroniki

Je sigara za kielektroniki na bidhaa nyingine zifananazo zina madhara?

WHO
Sigara ya kielektroniki

Je sigara za kielektroniki na bidhaa nyingine zifananazo zina madhara?

Afya

Kuna aina mbalimbali za sigara za kielektroniki kwa kiingereza Electronic Nicotine Delivery Systems au (ENDS), zikiwa na kiwango mbalimbali cha kichangamsho aina ya Nicotine na moshi hatarishi.

Moshi utokanao na sigara hizi huwa na Nicotine na dutu zenye sumu kwa wavutaji na wale wanaovuta moshi wa mvutaji wa sigara hizo. Baadhi ya vifaa vya kuvutia sigara hizo za kielektroniki ambavyo hudaiwa kuwa havina kemikali ya Nicotine vimebainika kuwa na kemikali hiyo.

Hakuna shaka yoyote kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu na si salama, lakini ni mapema mno kutoa jibu dhahiri juu ya madhara ya muda mrefu ya kutumia sigara hizi au kuvuta moshi wake.

Sigara hizi ni hatari zaidi zinapotumiwa na barubaru. Nicotine ina kiwango kikubwa sana cha uraibu na ifahamike kuwa ubongo wa vijana huendelea kukua hadi wanapotimiza umri wa miaka ya kati ya 20. Kukumbana na nicotine kunaweza kuwa na madhara ya muda mrefu.

Vijana wanaotumia sigara za kielektroniki wako katika uwezekano mkubwa zaidi wa kuvuta sigara za kawaida, biri au buruma.

Kama hiyo  haitoshi, sigara za kielektroniki zinaongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mapafu. Kwa wajawazito, sigara za kielektroniki zinaweza kuhatarisha makuzi ya mtoto tumboni.

Na si hivyo tu, sigara za kielektroniki si hatari kwa mvutaji peke yake bali pia wale waliokaribu naye watajikuta wanavuta moshi huo wenye kemikali ya nicotini na nyinginezo za sumu.

Mwanaume akivuta sigara katika eneo lililotengwa kwa ajili ya wavuta sigara kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.
UN News/Yasmina Guerda
Mwanaume akivuta sigara katika eneo lililotengwa kwa ajili ya wavuta sigara kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.

Majimaji yaliyomo kwenye sigara hiyo ya kielektroniki yanaweza kuunguza ngozi na kusababisha sumu hiyo iwapo itamezwa au itaingia mwilini kupitia kwenye ngozi. Kuna hatari pia ya kifaa hicho cha kuvutia sigara kikavuja au mtoto kumeza maji hayo na pia sigara hizo zimeshakuwa chanzo cha majeraha kutokana na moto au milipuko.

Je Sigara za Kielektroniki zinajeruhi mapafu?

Kuna ushahidi unaozidi kuonesha kuwa sigara za kieletrokoniki zinaweza kudhuru mapafu.

Tarehe 17 mwezi Septemba mwaka 2019, kituo cha Marekani cha kudhibiti na kukinga magonjwa, CDCP kilianzisha uchunguzi wa dharura wa uhusiano kati ya matumizi ya sigara za kielektroniki na madhara ya mapafu na vifo.

Hadi tarehe 10 mwezi Desemba mwaka 2019, Marekani ilikuwa imeripoti zaidi ya watu 2409 waliolazwa hospitali na vifo 52 vilivyothibitishwa kuhusiana na matumizi ya sigara hizo.

Takribani mataifa mengine 5 yameanza uchunguzi wa kubaini wagonjwa wa mapafu wanaohusiana na matumizi ya sigara za kielektroniki.

Je sigara za kielektroniki ni hatari zaidi kuliko zile za kawaida?

Hii hutegemea na vigezo mbalimbali ikiwemo kiwango cha nikotini na kemikali nyingine za sumu zinazochomwa pamoja, lakini yafahamika kuwa sigara za kielektroniki zina madhara dhahiri kwa afya na bila shaka si salama.

Je sigara hizi za kielektroniki zina  uraibu?

Ndio! Nicotini ni kemikali yenye kiwango cha juu sana cha uraibu. Na matumizi ya sigara za kieletroniki yanahusisha uvutaji wa kemikali hii ya nikotini.

 

Je wavutao moshi wa wavutaji sigara hizi za kielektroniki nao wako hatarini?

Ndio! Kemikali kwenye sigara ya kieletroniki zina dutu zenye sumu ikiwemo glycol ambayo hutumika kutengenezea kishushamgando au antifreeze. Sigara za kielektroniki ni hatari kwa watumiaji na wasiotumia.

Je sigara hizi za kielektroniki zipigwe marufuku?

Nchi zinaweza kuamua kupiga marufuku sigara hizo za kielektroniki.

Tayari sigara hizi zimepigwa marufuku katika mataifa zaidi ya 30 duniani kote, ambapo nchi nyingi zaidi zinafikiria kuchukua hatua kulinda vijana.

Kibao cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara kwenye eneo la bustani ya  mboga katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani.
UN News/Yasmina Guerda
Kibao cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara kwenye eneo la bustani ya mboga katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Je kuwepo na kanuni za matumizi ya sigara za kielektroniki?

Ndio! Sigara za kielektroniki ni hatari kwa afya na ambako bado hazijapigwa marufuku basi kanuni za udhibiti ziwekwe.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO linapendekeza kuwa nchi zitekeleza mikakati ya usimamizi ambayo inaendana na mazingira ya nchi husika.

Kanuni hizo zinapaswa:

·kutibua matangazo na matumizi ya bidhaa za sigara za kielektroniki;

· kupunguza hatari zitokanazo na matumizi ya sigara za kielektroniki kwa watumiaji na wasiotumia;

· kuzuia madai ya uongo au yasiyothibitishwa kuhusu sigara za kielektroniki; na,

·kulinda juhudi zilizopo za kudhibiti matumizi ya tumbaku.

Takribani ladha 15 000 za kipekee hutumika kwenye sigara hizo za kielektroniki ikiwemo zile zinazolenga kuwavutia vijana, kama vile ladha ya ubani au chingamu.

Serikali zinapaswa kudhibiti matangazo ya sigara hizo na pia ufadhili utokanao na sigara hizo ili vijana na makundi mengine hatarini na wasio wavutaji wasilengwe.

Matumizi ya sigara hizo maeneo ya ndani ya umma na maofisini lazima yapigwe marufuku kwa kuzingatia hatari zake kwa wale wasiovuta.

Kutoza kodi sigara hizi kama ilivyo kwa bidhaa za tumbaku itakuwa na manufaa kwa serikali na wakati huo huo kulinda raia kwa kuwa bei itakuwa juu na hivyo kudhibiti matumizi.

Juhudi za kupunguza matangazo ya Sigara kama haya zinaendelea kote duniani ili kupunguza ufutaji wa sigara ambao una athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazingira.
Maggie Murray-Lee
Juhudi za kupunguza matangazo ya Sigara kama haya zinaendelea kote duniani ili kupunguza ufutaji wa sigara ambao una athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazingira.

Je sigara za kielektroniki hukusaidia kuacha kuvuta sigara?

Hakuna ushahidi wa kutosha kuwa matumizi ya sigara hizi husaidia wavutaji wa sigara za kawaida kuacha kuvuta sigara.

Kwa wavuta tumbaku ambao wanataka kuacha kuvuta tumbaku, kuna njia zilizothibitishwa, salama na zilizoridhiwa kama vile tiba za kuondokana na nikotini, ujumbe kwa ya simu, na tiba mahsusi za kuondokana na uraibu wa tumbaku.

Je WHO inafanya nini kuhusu sigara za kielektroniki?

Mara kwa mara WHO inafuatilia na kutathmini sigara za kielektroniki na uhusiano wake na afya na kutoa ushauri kwa serikali na umma.

Hii ni pamoja na ripoti ya kila baada ya miaka miwili ya WHO kuhusu janga la tumbaku, ambayo  hufuatilia hali ya janga la tumbaku na hatua za kudhibiti pamoja na rasilimali zingine.

WHO inhaha kujenga dunia salama, yenye afya kwa kila mt una popote pale alipo.