Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMO inataka nchi kuhamasisha wanawake kuingia sekta ya usafirishaji wa majini

Takwimu za sasa zinakadiria kuwa idadi ya wanawake katika sekta ya usafirishaji wa majini ni asilimia mbili tu ya nguvu kazi yote ya sekta hiyo
Uto ni Yalo Trust/Samuela Ulacake
Takwimu za sasa zinakadiria kuwa idadi ya wanawake katika sekta ya usafirishaji wa majini ni asilimia mbili tu ya nguvu kazi yote ya sekta hiyo

IMO inataka nchi kuhamasisha wanawake kuingia sekta ya usafirishaji wa majini

Wanawake

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya usafirishaji majini, wito umetolewa kuongeza idadi ya wanawake katika tasnia hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la kimataifa la shughuli za usafirishaji wa majini IMO,  maadhimisho ya mwaka huu ni fursa ya kukuza uelewa wa umuhimu wa usawa wa kijinsia kuendana na Malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs na pia kusisitiza umuhimu wa mchango wa wanawake katika sekta ya usafirishaji wa majini.

Kihistoria tasnia ya usafirishaji  wa majini kwa miaka mingi imehodhiwa na wanaume, hata hivyo IMO inaamini kwa kuwawezesha wanawake kunachochea uchumi, kunakuza uzalishaji na tija pamoja na kufaidisha kila mdau katika jamii ya usafirishaji wa majini, kama anavyosisitiza Kitack Lim ambaye ni Katibu Mkuu wa IMO, “Usafirishaji majini mara zote umehodhiwa na wanaume kama ilivyo katika kazi nyingine zinazohusiana na tasnia hii ya usafirishaji kwa njia ya maji. Lakini hii inabadilika na kuna sababu nyingi za kwa nini. Usawa wa kijinsia umetambuliwa kama moja ya njia muhimu ambayo watu wanaweza kuzitumia kujenga mstakabali endelevu.”

IMO kupitia programu yake ya usawa wa kijinsia na pia ukuzaji wa uwezo hususani kwa wanawake, inahamasisha nchi wanachama wake kuwawezesha wanawake kupata mafunzo pamoja na wanaume katika vyuo vyao vya ubaharia ili waweze kufikia uwezo wa juu unaohitajika katika tasnia hiyo.

Takwimu za sasa zinakadiria kuwa idadi ya wanawake katika sekta ya usafirishaji wa majini ni asilimia mbili tu ya nguvu kazi yote ya sekta hiyo.