Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chakula kipoteacho baada ya mavuno Afrika chaweza lisha mamilioni- FAO

Wakulima Nigeria wajivunia mazao(Mtama)ya shamba lao.Picha: FAO

Chakula kipoteacho baada ya mavuno Afrika chaweza lisha mamilioni- FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Chakula kinachopotea shambani baada ya mavuno hususani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni kingi, na kinachangia hasara za kiuchumi na kijamii. Sasa shirika la chakula na kilimo FAO limeamua kulivalia njuga suala hilo.

Umoja wa Mataifa na wadau wake, wamechukua hatua kuondokana na chakula kinachopotea baada ya mavuno shambani hususan kwenye nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba chakula hicho kinachopotea baada ya mavuno kinaweza kulisha takribani watu milioni 48.

Kupotea kwa chakula baada ya mavuno kunahusisha kupungua kwa ubora na kiwango cha chakula kama vile nafaka, matunda, mboga, nyama, maziwa na samaki, tangu mazao hayo yanatoka shambani na kabla ya kuuzwa ili kumfikia mlaji.

 

Image
Mwanamke anakagua mpunga ulioongezewa virutubisho kwa ajili ya kupata mazao mengi. Picha: FAO/Daniel Hayduk

Barani Afrika, kiwango kikubwa cha chakula hupotea kati ya mavuno na mauzo, ambapo ni kiwango kidogo sana kinapotea baada ya mlaji kununua chakula hicho.

Ni kwa mantiki hiyo shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, Muungano wa Afrika, AU na taasisi ya Rockfeller wameanzisha mradi wa kudhibiti upotevu huo wa chakula ifikapo mwaka 2030, sambamba na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Wadau hao watasaidiana kuimarisha sera na mikakati ya uvunaji na uhifadhi wa chakula katika nchi hizo za Afrika wakizingatia kuwa nchi za Afrika kupitia azimio lao la Malabo la mwaka 2014, waliazimia kupunguza kwa asilimia 50 kiwango cha chakula kinachopotea baada ya mavuno ifikapo mwaka 2025.

"Kazi yetu na taasisi ya Rockfeller na Muungano wa Afrika ni kufanya mfumo wa chakula kuanzia shambani hadi mezani unakuwa thabiti Zaidi na unanufaisha vipato vya familia za wakulia,” amesema Jose Graziano da Silva, Mkurugeni Mkuu wa FAO akiongeza kuwa kwa kufanya hivyo wanaondoa shinikizo kwenye mazingira na hivyo kuchangia katika dira ya kutokomeza njaa duniani.

 

Image
Wakulima wadogo wadogo ndio wanatoa mazao mengi na kuhakikisha uwepo wa chakula nchini nzima. Picha: FAO

Mradi huo wa miezi 18 ulianza mwezi Februari mwaka 2017 na unalenga kudhibiti kupotea kwa mazao yanayotegemewa zaidi katika nchi za Kenya, Tanzania, Zambia na Zimbabwe pamoja na  usaidizi wa kisera kwa kamisheni ya Muungano wa Afrika.

Rafael Flor ni Mkurugenzi kutoka taasisi ya Rockfeller, anafafanua Zaidi kile wanachofanya kudhibiti upotevu wa chakula..

(Sauti ya Rafael Flor)

“Njia zinazotekelezeka ambazo unaweza kuchukua ikiwemo mifuko ya nailoni isiyoingiza hewa kabisa ambamo kwamo unahifadhi nafaka kwa muda mrefu na bila kupoteza lishe yake na inahifadhika kwa ubora zaidi. Unaweza kutumia makasha kusafirisha mazao kutoka shambani bila kuharibika. Lakini hii inahitaji mfumo wa hali ya juu na si teknolojia moja pekee. Inahitaji mfumo unaounganika kuanzia shambani, soko bora, njia bora za usafirishaji na mazingira yanayoandaliwa na serikali ambayo itakuwa inaongoza kwenye uwekezaji wa jambo hili. ”

FAO na taasisi ya Rockfeller walitia saini udau kati ya mwaka 2016 ili kusaidia kufanikisha upatikanaji wa chakula Afrika na kuwaendeleza wakulima wadogo kwa kuwajengea uwezo wa kudhibiti upotevu na utupaji wa chakula.