Chukueni hatua kukomesha unyanyapaa dhidi ya wenye ukoma- UN

19 Juni 2018

Mataifa ni lazima yachukue hatua kukomesha unyanyapaa ulioenea na wa kitaasisi unaoelekezwa kwa watu walio na ukoma pamoja na familia zao, amesema mtaalam maalum kuhusu utokomezaji wa unyanyapaa dhidi ya watu walio na ukoma na familia zao, Alice Cruz.

Akiwasilisha ripoti yake ya kwanza kwa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, mtaalam huyo amesema mataifa yana sio tu  wajibu lakini yanahitajika kukabiliana na unyanyapaa dhidi ya watu walio na ukoma kwani kundi hilo limekumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki zao.

Aidha amesema wamenyimwa hadhi yao na haki zao za msingi, huku wakikabiliwa na lugha ya kuwanyanyapaa, kuwatenga, kutengana na familia na jamii zao ikiwemo watoto.

Bi. Cruz ameongeza kuwa kundi hilo limenyimwa huduma muhimu ikiwemo mbinu za kujipatia kipato, mali na makazi na kuzuiwa kupata elimu, kuzuiwa kuoa au kupata watoto na uhuru wao wa kutembea.

Isitoshe ameongeza kuwa watu walio na ukoma wananyimwa haki ya kushiriki masuala  ya umma huku wakikabiliwa na ukatili ikiwemo wa kisaikolojia.

Wengi wa watu hao wanafichwa na kukumbwa na ukatili na ukikwaji wa haki zao huenda ukatajwa kuwa  ‘vifo vya raia’.

Mtaalam huyo maalum ametolea wito mataifa kufuta sheria zinazobagua katika zaidi ya mataifa ishirini, pamoja na kuondoa vizuizi vinavyonyima watu walio na ukoma haki, vile vile imani za kidini na fikra potofu, utamaduni na dhana zinazochangia unyanyapaa huo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter