UN yalaani mashambulizi ya kigaidi kwenye mechi ya kriketi Afghanistan
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, amelaani mashambulizi ya kigaidi kwenye michezo ya kriketi katika mji wa Jalalabad hii leo yaliyokatili maisha ya watu 8 na kujehuri 55.
Bwana Tadamichi Yamamoto ambaye ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, amesema uchunguzi wa kina umebaini kuwa wahusika wa vitendo hivyo vya kigaidi walilipua mabomu 4 yaliopangwa kwa ustadi ili kufanya madhara makubwa kwenye mkusanyiko wa wanainchi waliokuwa wanashuhudia mechi ya kriketi baina ya timu hasimu ya kwenye uwanja wa nyumbani.
Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa , Bwana Tadamichi Yamamoto ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa, huku akiwatakia ahueni majeruhi wote, na kuitaka serikali kufanya uchunguzi ili kubaini wahusika kwani vitendo hivyo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu na Umoja wa Mataifa.
Mkuu huyo ameongeza kuwa wakati huu wa mfungu ni wakati ambapo wananchi wa Afghanistan waanahitaji amani. Hivyo jamii ya kimataifa kwa ushirikiano na wenyeji wanatakiwa kupinga vitendo hivyo, na kuruhusu mchakato wa amani ya kudumu kwa ajili ya mstakhabali muzuri wa wananchi wa Afghanistan.