Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kifo cha Jahangir, tumepoteza jemadari wa haki- Guterres

Mwendazake Asma Jahangir.
Picha:UN/Maktaba
Mwendazake Asma Jahangir.

Kifo cha Jahangir, tumepoteza jemadari wa haki- Guterres

Haki za binadamu

Tumepoteza jemadari wa haki za binadamu, hiyo ndio kauli aliyoitoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres baada ya habari za kifo cha Asma Jahangir kutangazwa Pakistan hii leo alikotoka na duniani kote.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Bwana Guterres amesema Bi Jahangir alikuwa ni mtetezi asiyechoka wa haki za watu wote na mpigania usawa iwe kwa wadhifa aliokuwa nao kama mwanasheria kwenye mfumo wa sharia wa Pakistan, kama mwanaharakati wa kiraia wa kimataifa au kama mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kuwa Asma mwerevu, anayezingatia misingi ya kazi, jasiri na mtu mwema.

Kufuatia msiba huo mzito Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki, wafanyakazi wenzie, wakiwemo wa Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia ambako kote alikuwa kiongozi wa kipekee.

Amesema Asma hatosahaulika kamwe.