Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana nchini Sudan Kusini kupokea mafunzo kuhusu amani na mapatano

Vijana nchini Sudan Kusini kupokea mafunzo kuhusu amani na mapatano

Huku asilimia 72 ya wakazi wa Sudan Kusini wakiwa chini ya umri wa miaka 30, Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni, UNESCO linaeleza kuwa ni bayana kwamba hatma ya taifa hilo iko mikononi mwa vijana.

Ili kuweza kulea kizazi kipya balozi wa uhusinao mwema wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya amani na uwiano Forest Whitaker ametangaza kuwa wakfu wake wa PeaceEarth Foundation utazindua mtandao wa amani nchini Sudan Kusini.

Amesema mtandao huo utabuniwa kupitia ushirikano na ofisi ya UNESCO mjini Juba , wizara ya utamaduni , michezo na vijana na pia kwa ushirikiano na makampuni ya Zain na Ericsson.

Vijana kutoka majimbo 10 nchini Sudan Kusini watapewa mafunzo na wataalamu wa kimataifa kuhusu utatuzi wa mizozo, uongozi na amani na pia kuhusu mapatano.

Wakfu wa PeaceEarth na UNESCO wanashirikina na wizara ya vijana kubuni vituo vyenye kompyuta kwenye miji mikuu ya majimbo yote nchini Sudan Kusini ili kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao.