Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uongozi wa kisheria unapaswa kuimarishwa na nchi kwa manufaa ya wote:Ban

Uongozi wa kisheria unapaswa kuimarishwa na nchi kwa manufaa ya wote:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema leo kuwa uongozi wa kisheria unapaswa kuimarishwa katika kila nchi kwa manufaa ya wote. Bwana Ban amesema hayo katika kikao maalum cha mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu uongozi wa kisheria. Katibu Mkuu amesema kuimarisha uongozi wa kisheria ni muhimu katika kila taifa kama ilivyo katika jamii ya kimataifa.

Amesema anajivunia kuona kwamba Umoja wa Mataifa unaendeleza uongozi wa kisheria katika zaidi ya nchi 150. Ametoa wito kwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kwanza katika kuhakikisha usawa katika utekelezaji wa sheria kwenye ngazi ya kitaifa na kimataifa, bila ubaguzi.

Ameitaka kila nchi pia kuhakikisha kuna viwango vya juu vya uongozi wa kisheria katika uamuzi wote, kila wakati, na kwamba uongozi wa kisheria uwe msingi wa kila vitendo vya serikali. Amezitaka pia nchi wanachama kukubali kudhibitiwa na mfumo wa Mahakama ya Haki ya Kimataifa.