Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini, mwenye kuongoza ile tume iliodhaminiwa na Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu madaraka ya kuchunguza ukweli wa hali ya mapigano yaliotukia karibuni katika Tarafa ya Ghaza, alikutana na waandishi habari wa kimataifa baada ya kuzungumza na KM Ban Ki-moon mjini Geneva ambapo aliarifu ujumbe wao bado upo katika harakati za awali za matayarisho ya safari ya kuzuru Ghaza. Alisema "amesikitishwa" kwamba mpaka sasa bado hawajapokea jawabu ya kuridhisha kutoka Serikali ya Israel juu ya ombi lao la kuzuru Israel kusini, na baadaye Ghaza, na kumalizia safari yao katika ile sehemu ya WaFalastina iliopo katika Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan. Goldstone alieleza kuwa ataitisha vikao vya hadhara kadha atakapozuru Mashariki ya Kati, ili kusikiliza ushahidi mbalimbali wa umma kuhusu uhasama uliopamba katika Tarafa ya Ghaza miezi michache iliopita. Alisisitiza kwamba pindi tume yao haitofanikiwa kufanyisha kikao hicho Mashariki ya Kati, tume italazimika kuitisha kikao Geneva. Shughuli za tume zinatarajiwa zikamilishwe mwisho wa Juni, na baadaye wataikabidhi jumuiya ya kimataifa ripoti ya uchunguzi wao mnamo tarehe 04 Agosti 2009.

 Bishow Parajuli, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya UM katika Myanmar, akijumuika na baadhi ya Wanabalozi waliopo Yangon, Ijumatano waliruhusiwa kuhudhuria mahakama ya taifa kusikiliza mashtaka dhidi ya Daw Aung San Suu Kyi, baada ya kupokea mwaliko rasmi kutoka Serikali ya Myanmar. Baadaye wajumbe watatu, waliowakilisha balozi za Singapore, Thailand (kama mwenyekliti wa Jumuiya Mataifa Wanachama wa ASEAN) pamoja na mwakilishi wa ubalozi wa Urusi (taifa ambalo mwezi Mei linaongoza shughuli za Baraza la Usalama katika Makao Makuu), walipatiwa idhini ya kuonana na Aung San Suu Kyi. Baada ya hapo mabalozi watatu hawa walikutana na Mratibu Mkaazi wa UM na kumuarifu juu ya mazungumzo hayo.

Elizabeth Byrs, Msemaji wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) Geneva aliarifu waandishi habari kwamba makadirio halisi ya UM yamethibitisha kwamba baina ya watu 80,000 mpaka 100,000 waliuwawa kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika Sri Lanka, ambayo yalichukua miongo mitatu. UNHCR, kwa upande wake, imeeleza kambi za wahamiaji wa dharura Sri Lanka zimefurika watu wanaobanana, hali ambayo imedhihirisha umma muhitaji unapatiwa huduma haba za msingi, kunusuru maisha, kutoka jumuiya za kimataifa. Kambi hizi za wahamiaji zinakabiliwa na matatizo ya afya na usafi, pamoja na upungufu mkubwa wa makazi ya kujistiri. UNHCR hivi sasa inaisaidia serikali kukabiliana na tatizo la makazi, kwa kujenga vibanda 10,000 ziada. Hata hivyo UNHCR imeripoti kutoridhika na vikwazo kadha ilivyoekewa na wenye mamlaka, vikwazo ambavyo vinawanyima uwezo wa kuwapelekea raia muhitaji misaada ya kihali, hasa katika eneo muhimu la uhasama wa karibuni katika wilaya ya Vavuniya.

Wawakilishi wa Ujumbe wa Baraza la Usalama unaotembelea Afrika walipokuwepo Monrovia, mji mkuu wa Liberia Ijumatano walikutana kwa mashauriano na Raisi Ellen Johnson Sirleaf pamoja na wawakilishi wa serikali wa vyeo vya juu. Mazungumzo yao yalilenga zaidi kwenye masuala ya amani, shughuli za usalama wa kitaifa, ufufuaji wa huduma za uchumi na maendeleo, kwa ujumla. Kadhalika walizingatia ratiba ya kuondosha vikosi vya ulinzi amani vya UNMIL kutoka Liberia katika siku zijazo. Vile vile ujumbe wa Baraza la Usalama ulifanya mazungumzo maalumu na viongozi wa wafanyabiashara Liberia, ikijumuisha wawakilishi wa kampuni mbili za kutengeneza vyuma duniani - Arcelor Mittal na Buchanan Renewable Energy - kampuni muhimu ambazo zinaisaidia Liberia kupata mapato na ajira.