Hapa na Pale
Shirika la UM Linalosimamia Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limetangaza taarifa yenye kufafanua, kinaganaga, kwamba haitoshiriki kamwe, kwenye shughuli za aina yoyote au kujihusisha na operesheni zinazoambatana na Bosco Ntangada, kiongozi wa kundi la wanamgambo katika JKK. MONUC ilikumbusha ya kuwa Ntangada sasa hivi ameshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) kwa makosa ya vita, ikijumlisha jinai ya kuajiri kimabavu watoto chini ya umri wa 15, waliolazimishwa kushiriki kwenye mapigano na uhasama.
KM ameripotiwa kuhuzunishwa sana na ripoti ya mashambulio ya wafanyakazi wawili wanaotumikia Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), yaliotukia Ijumatatu kwenye mji wa Quetta, Pakistan. Mmoja wa watumishi hawo, Syed Hashim aliuawa, na abiria mwenziwe, John Solecki alitekwa nyara baada ya gari yao kusimamishwa na watu wenye silaha. Dereva, Syed Hashim, ambaye alifanya kazi na UNHCR kwa miaka 18, alipigwa risasi na kufariki baadaye wakati akitibiwa majeraha katika hospitali ya Quetta. John Solecki, aliye mkuu wa ofisi ndogo ya UNHCR Quetta, kwa miaka miwili, alitekwa nyara na majambazi wasiojulikana. KM amelaumu, kwa lugha kali, mashambulio hayo na alikumbusha kwamba lengo halisi la watumishi wa UM, kama Syed Hashim na Solecki, wanapoajiriwa kazi, ni kutumikia umma wa maeneo wanapopelekwa kufanya kazi, kwa kulingana na maadili ya kiutu na Mkataba wa UM. KM ameitumia aila ya Hashim mkono wa taazia. Kadhalika, KM ametoa ombi la kutaka Solecki atolewe kizuizini haraka, na kuachiwa bila ya mateso.
Kai Eide, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, amearifu masikitiko yake makubwa baada ya ripoti ya kushambuliwa kwa kituo cha polisi katika jimbo la Uruzgan, kitendo kilichosababisha vifo na majeruhi kadha. Eide alisema kitendo hiki kinaonyesha dhahiri ya kuwa waliofanya mashambulizi hayo hawajali maisha ya wanadamu, wala hawahishimu matakwa ya jamii zao ya kuwa na taifa lenye kutekeleza haki kwa wote. Alisema umma wa Afghanistan, katika kila pembe ya nchi, wanahitajia haki na kuwa na vyombo vya sheria vinavyoaminika, na juhudi za kufunza polisi zimekusudiwa kukidhia mahitaji hayo kama inavyostahiki.