Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon Ijumanne asubuhi alikuwa na mazungumzo ya ushauri, ya faragha, na wawakilishi wa Mataifa Wanachama 15 wa Baraza la Usalama kuhusu safari yake ya Mashariki ya Kati, yenye madhumuni ya kuhamasisha makundi husika na uhasama uliozuka kwenye Tarafa ya Ghaza, kusimamisha mapigano haraka, kama ilivyopendekezwa na azimio nambari 1860 (2009), na baadaye kuyawezesha mashirika yenye kuhudumia misaada ya kiutu kukidhia mahitaji ya umma waathirika na mapigano.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti asilimia 60 ya umma wa Ghaza hauna umeme. Viloe vile OCHA imesema kiwanda cha umeme katika Ghaza mjini kimepigwa makombora yalioharibu vibaya zile spea zinazohitajika kuhudumia, kidharura, mahitaji ya wakazi wa eneo hilo la uhasama. OCHA inasema visima vyingi vya maji vimeharibiwa, ikichanganyika na zile pampu zinazotumiwa kusafishia mabomba ya maji machafu kutokana na ukosefu wa umeme, na pia nishati ya kuendeshea majenereta na upungufu mkubwa wa spea.

UM umeripoti WaFalastina nusu milioni wanaoishi katika Tarafa ya Ghaza, hawana uwezo wa kufikia maji safi na salama bado, ikijumlisha asilimia 60 ya wakazi wa Mji wa Ghaza. Kadhalika, asilimia 80 ya maji ya kunywa Ghaza hayafai kutumiwa, katu, na wanadamu, kwa kulingana na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Katika maeneo ya Beit Hanoun na Beit Lahiya, Ghaza kaskazini, imeripotiwa makaro yamefurika pomoni na maji machafu yamemwagikia mitaani! Vile vile WHO imeripoti Hospitali ya Watoto ya Dorah, katika Ghaza, Ijumatatu ililengwa makombora na kupigwa moja kwa moja. Licha ya uharibifu huo, watumishi wa hospitali wanaendelea kufanya kazi zao kuhudumia wakazi waathirika na uhasama na mapigano.

Ahmedou Ould Abdallah, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali ametoa mwito kwa raia wa Usomali kuchukua fursa ya kuondoshwa kwa vikosi vya Ethiopia, kutoka maeneo kadha ya mji wa Mogadishu, kurudisha utulivu na amani nchini. Aliwahimiza kukomesha tabia ya “kuua kihorera na kupalilia vurugu lisio na maana”; na kuwataka waendelee na matayarisho yao ya kuchagua Raisi mpya, na vile vile kuwanasihi wabunge wakithirishe idadi yao na kushirikiana kuunda serikali ya muungano, kwa masilahi ya muda mrefu ya taifa lao.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti Ijumanne idadi ya vifo vya kipindupindu katika Zimbabwe hivi sasa imefikia 2,000, baada ya kusajiliwa vifo 100 Ijumatatu na UM. Kadhalika ripoti ilibainisha karibuni wagonjwa 1,500 wapya waliambukizwa na maradhi hayo. Mpaka sasa WHO imethibitisha rasmi wagonjwa karibu 40,000 wameripotiwa kuambukizwa na kipindupindu katika Zimbabwe.

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa litaanza kupeleka misaada ya chakula kwa wahamiaji 250,000 wa Sudan waliopo Chad. Hivi sasa misafara ya malori ya WFP, yaliochukua misaada ya chakula, inavuka kilomita 2,800 kwenye jangwa la Sahara, kutokea Libya na unaelekea Chad kwa makusudio ya kuhakikisha wahamiaji wa Sudan waliopo huko watapata chakula, kabla ya majira ya mvua kuanza. Libya ilianza kusaidia huduma hizi za WFP tangu mwaka 2004.