Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inasema chuki za wageni Afrika Kusini zawahamasisha wahamiaji wakazi kurudi makwao

UNHCR inasema chuki za wageni Afrika Kusini zawahamasisha wahamiaji wakazi kurudi makwao

UM inashiriki kwenye huduma za kuwasaidia kurejea makwao wageni kadhaa waliong’olewa makazi Afrika Kusini, kwa sababu hawana furaha na maisha wanaoongoza nchini humo kwa sasa, hasa baada ya kufumka vurugu la chuki za wageni katika mwezi Mei lilioenea nchini humo kwa wakati huo.

Kwa mujibu wa Pamela Msizi, msaidizi wa miradi ya hifadhi ya UNHCR Afrika Kusini, alinakiliwa akisema kwamba kutokana na kufungwa kwa zile kambi za muda kwa wahamiaji wageni, na pia tabia ya kutotaka au kutoweza kujiunga na jamii za kienyeji, kulisababisha idadi kubwa ya wahamiaji hao kuingiwa na kiherehere juu ya maisha yao na walijionea ni bora warejee makwao badala ya hali hiyo ya wasiwasi. Bi Msizi alikusudia ule uamuzi wa wenye madaraka katika jimbo la Gauteng wa kuzifunga kambi sita za makazi ya muda kwa wageni 6,000 waliokimbia vurugu la chuki za wageni Afrika Kusini ndio ilioongeza wasiwasi waahamiaji hao. Lakini kambi hazikuweza kufungwa kwa sababu Mahakama ya Katiba Afrika Kusini iliamrisha uamuzi wa suala hilo uakhirishwe mpaka kutakapotolewa hukumu nyengine baadaye.

UNHCR imeripoti wiki hii kuwa imo mbioni kuwasaidia kuwarejesha makwao wale wahamiaji wageni wanaotaka kurejea kwa khiyari, pindi hali huko ni ya utulivu na amani. Kwa mfano, tarehe 18 Agosti UNHCR ilifanikiwa kuwasafirisha kwa ndege raia 46 walioomba kurejeshwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, pamoja na Waburundi sita waliotaka kurejea nchini kwao. Kadhalika, kundi jengine la Wakongo 23 na Waburundi tisa wanatazamiwa kurejeshwa makwao mwezi ujao, kwa msaada wa UNHCR. Hivi sasa UM unaendelea kupokea maombi ziada kutoka kwa wakazi wageni Afrika Kusini wanaotaka wasaidiwe kurejeshwa makwao. Kwa mujibu wa kanuni za UNHCR, shirika lipo tayari kurejesha kila atakaye kurudi nchini kwao, kwa khiyari, miongoni mwa wale wakazi wageni 128,000 waliosajiliwa Afrika Kusini, pamoja na wale walioomba hifadhi, pindi nchi walizotokea hazina vurugu na salama.