Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan

Ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan

KM wa UM Ban Ki-moon wiki hii alifanya ziara ya siku nne nchini Sudan, ikiwa miongoni mwa juhudi za kimataifa, kuleta hatima ya mgogoro na vurugu liliolivaa jimbo la magharibi la Darfur. Kadhalika, KM alichukua fursa ya kujionea binafsi aina ya mazingira yatakayovikabili vikosi mseto vya UM na Umoja wa Afrika wa AU vitkavyopelekwa Darfur mwakani.~

Baada ya Khartoum KM Ban alitembelea Juba, Sudan kusini na kuonana na Salva Kiir, Naibu Raisi wa Kwanza wa nchi, na alichukua fursa hiyo kushuhudia maendeleo yaliopatikana tangu Maafikiano ya Jumla ya Amani (CPA) kukamilishwa kati ya Sudan Kaskazini na Kusini. Alipokuwepo Juba KM pia alitangaza kumteua mwanadiplomasiya wa Pakistan, Ashraf Jehangir Qazi kuwa Mjumbe wake Maalumu mpya kwa Sudan.

Baadaye KM Ban alielekea El Fasher, mji mkuu wa jimbo la magharibi la Darfur, na huko alizuru makao makuu ya vikosi vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Afrika vya AMIS, na pia kuonana na Mjumbe Shirika wa AU-UM kwa Darfur, Rodolphe Adada pamoja na Kamanda Mkuu wa vikosi vya AMIS, Meja-Jenerali Martin Agwai. Kadhalika KM alikutana na wajumbe wanaowakilisha wahajiri wa ndani ya nchi.

Alkhamisi walipokuwepo mjini Khartoum, Raisi wa Sudan Omar al-Bashir na KM wa UM Ban Ki-moon walitangaza kuwa imekubaliwa kufufua tena mazungumzo ya amani kwa Darfur yatakayofanyika mwaka huu tarehe 27 Oktoba nchini Libya. Ni matarajio yao mazungumzo haya yatakamilishwa haraka na kwa mafanikio.