Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU linazungumzia suala la Darfur

BU linazungumzia suala la Darfur

Baraza la Usalama lilijadilia mapema wiki hii suala la Darfur ambapo Rodolphe Adada, Mjumbe wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa (UM) na Umoja wa Afrika (UA) kwa Darfur alihadharisha wajumbe waliokusanyika mkutanoni ya kuwa operesheni za ulinzi wa amani za Vikosi vya Kimataifa vya UNAMID katika jimbo la Darfur hivi sasa zinakabiliwa na matatizo magumu kwa kila hali, matatizo ambayo yanahitajia suluhu ya haraka.

Kadhalika, Naibu-Katibu-Mkuu juu ya Masuala ya Kiutu, John Holmes naye aliunga mkono bayana za Adada pale alipowakilisha mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama taarifa yake kuhusu hali katika Darfur. Holmes alisema amehuzunishwa, na kughadhibishwa sana kuona jumuiya ya kimataifa inashindwa kuwapatia mamilioni ya raia - waume, wake na watoto katika Darfur - suluhu ya kuridhisha na ya kudumu, baada ya miaka mitano ya mateso na mtafaruku, na miaka minne tangu pale Baraza la Usalama lilipojihusisha moja kwa moja na mzozo wa Darfur.

Alisema Holmes uenenzaji wa haraka wa vikosi ziada vya UNAMID ukitekelezwa sasa hivi katika Darfur huenda ukasaidia hali kidogo; lakini alionya pia hali huko haitotulia na wala afueni haitopatikana mpaka pale hali ya vurugu na matumizi ya mabavu dhidi ya raia yatakapokomeshwa, na pia itakapohakikishwa kuchukuliwa hatua thabiti kusawazisha tofauti za kisiasa zilizopo kati ya makundi husika na, hatimaye, kudumisha amani ya kuridhisha kwa wote katika Darfur, ukweli ambao makundi ya waasi ni lazima kuutambua, aliongeza kusema Holmes.