Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yachukua hatua kudhibiti waasi wa CODECO huko Ituri, DRC

MONUSCO yachukua hatua kudhibiti waasi wa CODECO huko Ituri, DRC

Pakua
Afya ya mlinda amani wa Umoja wa Mataifa aliyejeruhiwa katika shambulizi lilitekelezwa na kundi la waasi, CODECO juzi Agosti 28 huko Bali, kaskazini mashariki mwa Djugu jimboni Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaendelea vizuri. Anold Kayanda na maelezo zaidi.
 
Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaeleza waandishi wa habari jana Agosti 29 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kuhusu tukio hilo la kushambuliwa kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa katika shughuli zao za kuwahakikishia usalama raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
“Walinda amani walizuia shambulio hilo, na kuwalazimisha wanamgambo kuondoka. Hata hivyo, tunasikitika kuripoti kwamba mlinda amani mmoja alijeruhiwa.” Anaeleza Dujarric lakini akiwaondolea wasiwasi waandishi waliokuwa wakimsikiliza kwamba mlinda amani huyo aliyejeruhiwa sasa yuko katika hali nzuri.
Licha ya kushambuliwa, walinda amani wanaohudumu nchini DRC katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO wameendelea na shughuli za ulinzi si tu kaskazini mashariki mwa Djugu, bali pia kusini mashariki mwa eneo hilo jimboni Ituri ambako CODECO wameweka kambi katika maeneo mawili. Msemaji wa Katibu Mkuu anaeleza kwamba walinda amani walifanikiwa kusaidia raia wa kawaida kuweza kutoka eneo moja kwenda jingine.
Mashambulizi haya yanatokea ikiwa imesalia miezi michache kufika Desemba 31 mwaka huu ambayo ni tarehe iliyoridhiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba uwe mwisho wa MONUSCO kutokana na ombi la serikali ya DRC lilioomba MONUSCO iondoke katika nchi hiyo iliyogubikwa na vita kwa miaka mingi.  
Audio Credit
Cecily Kariuki/Anold Kayanda
Sauti
1'47"
Photo Credit
MONUSCO/Nazar Voloshyn