Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchafuzi wa udongo ni tishio kubwa kwa Mmustakhbali wa kilimo:FAO

Uchafuzi wa udongo unamulikwa. Picha: FAO

Uchafuzi wa udongo ni tishio kubwa kwa Mmustakhbali wa kilimo:FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Uchafuzi wa udongo ni tishio kubwa kwa uzalishaji wa kilimo , uhakika wa chakula na afya ya binadamu limeonya shirika la chakula na kilimo FAO.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya FAO iliyotolewa kwenye ufunguzi wa kongamano la siku tatu la kimataifa mjini Roma Italia, kuna ufahamu mdogo sana wa kiwango na ukubwa wa tishio hilo.

FAO inasema asilimi 95 ya chakula kinazalishwa kwenye udongo na hivyo kufanya uhifadhi wake na udhibiti endelevu wa udongo kuwa ni kitu muhimu sana ili kufikia takribani asilimia 50 ya ongezeko la uzalishaji wa chakula unaohitajika katikati ya karne hii ili kukidhi mahitaji.

Image
Wakulima nchini India wanapima kiwango cha maji kwenye udongo. Picha: FAO

Eduardo Mansur, ni mkurugenzi wa FAO wa idara ya ardhi na maji, anayehusika na mabadiliko ya tabia nchi na  bayoanuai , anafafanua kuhusu hali ya kimataifa ya udongo.

(SAUTI YA EDUARDO MANSUR)

“Udongo ndio shina kwa asilimia kubwa ya uszalishaji wetu wa chakula, Kwa muda mrefu tumekuwa hatuupi udongo thamani inayostahili kama chachu ya uzalishaji wetu wa chakula na kwa ajili ya lishe yetu, nadhani tunafikia kiwango ambacho tunahitaji kuuenzi zaidi udongo kwa sababu udongo wenye afya huzalisha chakula chenye afya”

Amesisitiza kuwa

(SAUTI YA EDUARDO MANSUR )

“Uchafuzi wa udongo ni adui aliyejificha , wakati mmomonyoko wa udongo unaweza kuuona, wakati kiwango cha chumvi katika udongo ni dhahri, uchafuzi wa udongo umejificha kwa kiasi kwamba wakati mwingine unabainika tu ikiwa tayari tumechelewa.”

Kongamano hili ni hatua ya kwanza katika kubaini na kuziba mapengo na kuchukua hatua za kimataifa kukabiliana na tishio litokanalo na uchafuzi na uharibifu wa udongo. Hatua hizo ni pamoja na kuandaa ajenda itakayochagiza utekelezaji wa muongozo wa FAO na wadau uliotolewa mwaka 2016 na mkakakati wa karibuni wa kimataifa wa kudhibiti ipasavyo uchafuzi wa udongo.

Kongamano hilo litakunja jamvi Ijumaa na linatarajiwa kutoka na mikakati ya kuhakikisha uchafuzi wa udongo unadhibitiwa kwa ajili ya mustakhbali wa uhakika wa chakula na watu wanaokitumia.