Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Ripoti SOFI: Watu takriban milioni 733 walikabiliwa na njaa 2023

UN Ripoti SOFI: Watu takriban milioni 733 walikabiliwa na njaa 2023

Pakua

Takriban watu milioni 733 walikabiliwa na njaa mwaka 2023, hii ikiwa ni sawa na mtu 1 kati ya 11 duniani na mtu mmoja kati ya watano barani Afrika, kulingana na ripoti mpya ya Hali ya Uhakika wa Chakula na Lishe Duniani SOFI, iliyochapishwa leo na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa. 

Ripoti hiyo ya kila mwaka iliyozinduliwa nchini Brazili katika mkutano wa mawaziri wa nchi 20 zenye kipato cha juu duniani  au G-20 imeonya kwamba  dunia iko mbali sana kufikia lengo la 2 la Maendeleo Endelevu, la kutokomeza njaa, ifikapo mwaka 2030.

Pia inafichua kwamba dunia imerudi nyuma miaka 15, huku viwango vya utapiamlo vikilinganishwa na vile vya mwaka  2008-2009.

Ripoti inasema licha ya maendeleo kiasi yaliyopigwa katika maeneo maalum kama vile kudumaa na kunyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee, viwango vya njaa duniani vimedorora kwa miaka mitatu mfululizo, na mwaka 2023, kulikuwa na watu milioni 152 zaidi wenye utapiamlo kuliko mwaka 2019.

Kwa mmujibu wa mashirika matano ya Umoja wa Mataifa yaliyoandaa ripoti hiyo lile la chakula na kilimo FAO, la mpangowa chakula duniani WFP, la ufadhili wa maendeleo ya kilimo IFAD, la kuhudumia  watoto UNICEF na la afya duniani WHO bara linaloongoza kwa ongezeko la watu wenye njaa ni Afrika kwa asilimia  20.4, Asia  asilimia 8.1 na Amerika ya Kusini asilimia 6.2.

Ripoti hiyo imegawanyika katika  sehemu tatu: Mosi viasharia vya njaa ambapo inasema upatikanaji wa chakula unaendelea kuwa mtihani kwa mamilioni ya watu, ukosefu wa fursa za kiuchumi za kupata mlo kamili ni changmoto kubwa ,watoto kuzaliwa na uzito mdogo na kudumaa ni matatizo sugu na katika muongo uliopita kumekuwa na ongezeko kubwa  la utipwatipwa.

Pili  imetaja sababu za ongezeko la njaa kuwa ni  mfumuko wa bei, vita na mabadiliko ya tabianchi.

Na tatu nini kifanyike: Ripoti inapendekeza uwekezaji ili kufadhili kukomesha njaa, uhaba wa chakula na aina zote za utapiamlo.

Na imeonya kwamba ikiwa hali ya sasa itaendelea, takriban watu milioni 582 watakuwa na utapiamlo sugu ifikapo 2030, nusu yao wakiwa barani Afrika.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
© UNICEF/Olivia Acland