Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baadhi ya wapalestina warejea kwenye nyumba zao zilizoathiriwa na mabomu baada ya kulazimishwa kuondoka Rafah

Baadhi ya wapalestina warejea kwenye nyumba zao zilizoathiriwa na mabomu baada ya kulazimishwa kuondoka Rafah

Pakua

Kuongezeka kwa shughuli za kijeshi huko Rafah, kusini mwa Gaza, kumesababisha mamia kwa maelfu ya watu kuyahama makazi yao, na kufanya maisha kuwa magumu zaidi kwa maelfu ya familia ambazo tayari zimelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP lina wasiwasi mkubwa kwamba hali hii ya kuhama hama inaweza kusababisha janga la kibinadamu, nakupelekea kusimama kwa shughuli za kutoa misaada ya kibinadamu.

Baada ya kufika nyumbani kwake, Ibrahim Kamal Ibrahim Amtair anamuonesha mtoto wake mdogo wa kike box lililojaa bidhaa mbalimbali za msaada aliopokea kutoka WFP. 

Ibrahim ni mmoja wa watu waliokimbia makazi yao Khan Younis na kukimbilia Rafah baada ya amri ya Jeshi la Israel lakini baada ya Israel wiki iliyopita kutoa tena amri ya kuwataka kuondoka Rafah ameona hana tena pa kukimbilia na kuamua kurejea katika nyumba yake. 

Amekuta nyumba yake imeathirika vibaya na mabomu pamoja na risasi, baadhi ya maeneo hakuna madirisha wala milango huku kukiwa na matundu ambayo ameyafunika kwa mabox na anasema mpango wake ni kukarabati matundu hayo ili watoto wake wasijeumia. 

“Hawakusema kuwa eneo hili liko salama, lakini tumerudi kwa sababu hatuna mahali pa kwenda, na hatukuwa sawa katika maeneo tuliyokuwepo. Hakuna anayejisikia raha isipokuwa akiwa nyumbani kwake, hata kama nyumba ikiwa imeharibiwa.”

Mbali na chakula cha msaada pamoja na vifurushi vya msaada wanavyo patiwa wananchi wa Palestina ambavyo vina vyakula kama vile makopo ya maharage, mbaazi na nyama ya kopo, Mkurugenzi wa WFP huko Palestina, Matthew Hollingworth anasema hifadhi iliyopo sasa ya chakula na mafuta itaisha baada ya siku chache.

“Hatujaweza kufikia ghala letu huko Rafah kwa zaidi ya wiki moja sasa. Tuna chakula kidogo na mafuta yanayokuja kupitia vivuko vya mpaka kusini na tunajitahidi kila wakati lakini tunashindwa kwa sasa kuleta kiasi cha kutosha cha chakula. Tunajua, tunahitaji njia za ziada za kuingilia na kila njia ya kuingilia ni mshipa wa kusukuma damu kuingia Gaza. Kwahiyo, tutafanya kazi kwa bidii ili kuendelea kupata njia mpya za kuingia na kupata usaidizi zaidi, kwa wingi na mara kwa mara ili kusaidia kukomesha njaa ambayo inajongea.”

Pamoja na changamoto nyingi, WFP inaendelea kusalia Gaza na kushirikiana na wadau wengine katika kutoa msaada kwa wapalestina.

Audio Credit
Thelma Mwadzaya
Audio Duration
2'32"
Photo Credit
© WFP/Arete/Abood al Sayd