Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili ombi la Palestina kuwa mwanachama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili ombi la Palestina kuwa mwanachama

Pakua

Huko Gaza, watoa misaada ya kibinadamu wakiwa na wasiwasi mkubwa juu ya mipango ya Israel kuvamia eneo la Rafah hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa Palestina imeanza mchakato wa kuwa mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa kwani hivi sasa ujumbe wake ni uangalizi usioipatia hadhi ya kupiga kura. Mchakato huo unaanzia ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Ratiba ya mikutano hii leo hapa katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa Baraza la Usalama lenye wajumbe 15 kuanzia saa nne kamili asubuhi mpaka saa sita kamili mchana kwa saa za New York Marekani, litakutana kwanza katika kikao cha faragha na kisha kikao kitafunguliwa kwa umma kusikiliza wanapojadili ombi la Palestina kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Palestina imekuwa ikishiriki katika masuala mbalimbali ndani ya Umoja wa Mataifa lakini kwa ngazi ya muangalizi na sasa uongozi wa Palestina inataka hadhi hiyo kubadilishwa na kuwa mwanachama kama wanachama wengine 193 wa Umoja wa Mataifa.

Wajumbe katika baraza hilo la UN katika mazungumzo yao watazingatia ombi la Wapalestina la mwaka 2011 baada ya ombi lililowasilishwa kwa njia ya maandishi wiki iliyopita na Bwana Riyad Mansour, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Palestina ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa.

Wakati tukisubiri kusikia nini kitajadiliwa na Baraza hilo, huko Ukanda wa Gaza hali bado si hali kwani watoa misada ya kibinadamu wana wasiwasi mkubwa juu ya uvamizi unaopangwa kufanywa na Israel katika eneo la Rafah ambalo limefurika wapalestina waliokimbia kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo kusini, kati na kaskazini mwa Gaza kufuatia mapigano yanayoendelea baina ya wanamgambo wa kipalestina wa Hamas na wanajeshi wa Israel.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, Jamie McGoldrick, akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa hapo jana alisema kuwa “Mpango unaendelea wa uvamizi wa Rafah, ambao unaweza kusababisha hadi watu 800,000, kuyakimbia makazi yao…. Tulipata tabu sana kuleta mahitaji muhimu hapa kama vitu ambavyo si vyakula, malazi, nyenzo mbalimbali na maji…. Hatuna tena uwezo na rasilimali kwa sasa. Na tunatatizika sana kujiandaa.”

Ili kuongeza kiwango cha usaidizi wa kibinadamu kufika eneo hilo, Umoja wa Mataifa unaunga mkono wito wa bandari ya Ashdod ya Israel kufunguliwa tena hulo kaskazini mwa Gaza, ili misaada zaidi ipatikane kupitia nchi ya Jordan.

Audio Credit
Leah Mushi
Sauti
2'24"
Photo Credit
UN News/Ziad Taleb