Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mariam Suleiman: Wanawake tuna ujuzi, tuna uweo na tunaweza

Mariam Suleiman: Wanawake tuna ujuzi, tuna uweo na tunaweza

Pakua

Mwanamke akiwezeshwa anaweza, huo ndio umekuwa usemi wa Umoja wa Mataifa ukipigia chepuo wanawake kujumishwa katika kila Nyanja ya Maisha ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya jamii. Usemi huo unaungwa mkono na mwanamke mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambaye sasa anaishi Kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya. 

Kutana na Mariam Suleiman ambaye kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR anasema vita ilimfungisha virago Congo DRC hadi hapa kambini Kakuma, ingawa ilimvurugia amani yake haikumkatishia ndoto zake za kuendelea na ufundi wa kuchomelea vyuma na pia kuwa mkufunzi wa kazi hiyo.

“Katika kuchomelea vyuma ninafurahia sana kufanyakazi kazi hiyo ninapokwenda kazini na kujikuta ni mwanamke peke yangu uwanjani na hivyo ninajivunia sana kwa sababu sio kazi rahisi kwenda hapo ukiwa mwanamke peke yako katikati ya wanaume 15. Hivyo ninajivunia sana kuwa mchomelea vyuma na mkufunzi wa kuchomelea na kutengeneza vyuma”

Kwa Mariam matunda ya kazi yake yako dhahiri.

“Moja ya kazi zangu zinazovutia ambazo nimefanya ni lango kuu  la kliniki 4”

Pamoja na mafanikio hayo Marian anatamani kusoma zaidi kuongeza ujuzi.

“Nilisoma hadi daraja la sita hiyo ni ngazi ya Diploma. Natamani kuchimba ndani zaidi ya hii tasnia ya kuchomelea vyuma lakini hapa Kenya hatuna hiyo kozi. Ipo katika taasisi ya uchomeleaji vyuma ya Afrika Kusini. Ningependa kwenda huko na kusoma uchomeleaji vyuma chini ya maji.”

Na kwa kuwa yeye ameweza anaamini hakuna kinachomshinda mwanamke kwani

“Wanawake tuna uwezo, wanawake tuna ujuzi, wanawake tunaweza kufanyakazi zinazofanywa na wanaume, wanawake tunaweza kufurahia kazi zetu, wanawake hebu tusimame kidete tunaweza”

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'7"
Photo Credit
Picha/Siegfried Modola