Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyumba salama kwa waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan Kusini

Nyumba salama kwa waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan Kusini

Pakua

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS kwakushirikiana na wadau wake wamefungua nyumba salama huko Andari Magharibi katika jimbo la Equatoria kwa ajili ya kusaidia manusura wa unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro nchini humo. Leah Mushi na maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa zamani wa UNMISS ofisi ya Yambio, Christopher Muchiri Murenga, mradi huu ulioanzishwa na kitengo cha ushauri cha ulinzi wa wanawake cha UNMISS na umefadhiliwa na Muungano wa Ulaya pamoja na Shirika la Rural Action Aid lengo likiwa ni kuwasaidia waathirika wa unyanyasji wa kijinsia unaohusiana na migogoro.

Bwana Murenga anasema, “kama sehemu ya kutafuta amani ya kudumu na jumuishi nchini Sudan Kusini, imebidi tuwalete manusura pamoja ili waweze kuponya majeraha yao. Kisha watakuwa wanajamii wenye tija, wakichangia ustawi wa kijamii na kiuchumi wa serikali.”

Kituo hiki kinatoa ushauri nasaha, kuponya watu wenye kiwewe pamoja na mafunzo ya stadi za maisha na kinalenga kusaidia manusura 195. Mmoja wa wanufaika ni Azande ambaye katika video ya UNMISS amefichwa sura yake wakati akieleza masahibu aliyopitia akisema, “tulipotoka porini nilikuwa na kiwewe, walitupa ushauri nasaha na mawazo yote mabaya yaliyokuwa akilini mwangu yaliondoka na sasa niko thabiti zaidi. Mimi ni miongoni mwa wale ambao sasa wanajifunza ushonaji. Wakati nipo msituni nilijifungua mtoto wa kike sasa ana umri wa miaka 6. Ana matatizo ya tumbo kwa sababu wakati mjamzito nilikuwa nakula vitu vya hatari ndio maana sasa naomba msaada wa dawa kwa ajili yake.”

Kiongozi wa kikundi cha wanawake katika eneo la Ezo Henrica Elias anasema nyumba hii itasaidia wasichana na wanawake wengi sana kwa kuwa, “kituo hiki ni kama ndoto inayotimia, imetuletea furaha ambayo hatuwezi kuieleza. Yaliyotusibu sisi wanawake na wasichana wakati wa mzozo ni yakutisha. Mambo mengi mabaya yalitendeka katika vijiji vyetu, ambapo wasichana wadogo na wavulana pia walitekwa nyara.”

Migogoro nchini Sudan Kusini imesababisha tajriba ya kuhuzunisha kwa vijana wengi wa kike na wa kiume, hasa wale ambao walilazimika kujiunga na makundi yenye silaha nchini humo.

Audio Credit
Anold Kayanda/Leah Mushi
Sauti
1'55"
Photo Credit
UNMISS