Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Tekelezeni kikamilifu mkataba wa mwaka 1994 wa kuwalinda wafanyakazi wa UN

Guterres: Tekelezeni kikamilifu mkataba wa mwaka 1994 wa kuwalinda wafanyakazi wa UN

Pakua

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa Walio vizuizini na wasiofahamika waliko, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa ulimwengu kuenzi ujasiri na kujitolea kwa wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu kila mahali kokote waliko kwa kuahidi kuwalinda na kuwaunga mkono wanaposaidia kujenga dunia yenye amani zaidi na ya utu kwa ajili ya watu wote. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Siku hii ya Kimataifa ya Mshikamano na Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa Walio vizuizini na wasiofahamika waliko huadhimishwa kila mwaka Machi 25 katika kumbukumbu ya kutekwa nyara kwa Alec Collett, mwandishi wa habari wa zamani ambaye alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) wakati alipotekwa nyara na mtu aliyekuwa na silaha mwaka wa 1985 na baadaye mwili wake kupatikana katika Bonde la Bekaa nchini Lebanon mwaka wa 2009 yaani miaka 24 baadaye.

Maadhimisho ya siku hii, katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa hata ana umuhimu mkubwa zaidi kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu Guterres kupitia ujumbe wake kwa maadhimisho ya mwaka huu anatoa takwimu za hivi karibuni akieleza kwamba tangu mwaka juzi 2022, wafanyakazi 381 wa Umoja wa Mataifa wamewekwa kizuizini ikiwa ni pamoja na wafanyakazi 7 mnamo mwezi Januari na Februari mwaka huu 2024. Kwa jumla, wafanyakazi 27 wa Umoja wa Mataifa bado wako kizuizini.

Bwana Guterres anasema leo ni ukumbusho mzito wa hatari kubwa zinazowakabili wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanapofanya kazi yao muhimu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa na kwamba, "Mioyo yetu iko pamoja na familia zao na wafanyakazi wenzao”, na kwamba hatakataa tamaa kutaka waachiliwe na kurudi salama."

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa anazisihi nchi zote kutekeleza kikamilifu Mkataba wa mwaka 1994 wa Usalama wa Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Washirika wao, na pia Itifaki ya Hiari ya mwaka 2005 ya Mkataba huo.

Audio Credit
Anold Kayanda/Assumpta Massoi
Sauti
1'45"
Photo Credit
Shpend Bërbatovci