Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO: Baa la njaa lanyemelea Gaza

FAO: Baa la njaa lanyemelea Gaza

Pakua

Hali ya uhakika wa kupata chakula huko Gaza, ni tete na baa la njaa linanyemelea kwenye majimbo ya kaskazini mwa eneo hilo imesema ripoti mpya ya  hali ya chakula Gaza iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, likisema jawabu la kuondokana na hali hiyo ni amani. 

Rein Paulsen, Mkurugenzi wa Ofisi ya Masuala ya Dharura na Mnepo FAO akizungumza hii leo huko Roma, Italia wakati wa kutolewa kwa ripoti hiyo ya uchambuzi wa viwango vya uhakika wa kupata chakula au IPC kwa Ukanda wa Gaza, anasema takwimu zinajenga taswira ya hali ya kutia wasiwasi mkubwa. Na pindi tunapofikiria kuhusu Gaza Kaskazini, ambako hali ni mbaya zaidi, uchambuzi wa sasa  unatuonesha kuwa njaa ni dhahiri katika kipindi cha kuanzia sasa na Mei 2024.

Hii ina maana tunapotazama mwelekeo wa takwimu za hali ya upatikanaji chakula na lishe tunaona hali ya kutisha. Kusini, hali nayo imezidi kuwa mbaya na huko tunashikilia makadirio yetu ya uwezekano wa baa la njaa.”

Ripoti inaonesha kuwa mwendelezo wa uhasama umesambaratisha sekta ya kilimo, ambayo familia za Gaza inategemea kwa ajili ya kujipatia kipato.

“Watu wote kwenye ukanda wa Gaza wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu mkubwa wa chakula ukiwekwa katika kiwango cha 3, na 4. Hii inaamanisha nusu ya idadi ya watu wote wa eneo hilo, takribani milioni 1.1 wanaweza kukabiliwa na janga kubwa la ukosefu wa uhakika wa chakula la kiwango cha 5.”

Hivyo amesema usaidizi wa haraka unahitajika kurejesha uzalishaji wa chakula na kwa mujibu wa ripoti

“Inatueleza kuwa baadhi ya mifugo iko hai, na inaweza kusaidiwa na ndio maana FAO inajikita kusaidia mahitaji ya kujipatia kipato Ukanda wa Gaza. Kwa sasa tumepata kibali cha kupeleka tani 1500 za ujazo za chakula cha mifugo.”

Amesema uhai wa mifugo utakuwa hakikisho la upatikanaji wa maziwa kwa familia, maziwa ambayo yatakuwa ni lishe bora kwa watoto na hivyo kukabili utapimlo uliokithiri miongoni mwa watoto.

Akatamatisha akisema, “uhakika wa kupata chakula utawezekana kukiweko na amani. Na haki ya kupata chakula ni haki ya msingi. Hili linapaswa kuzingatiwa na wadau wote.”

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
2'7"
Photo Credit
© UNRWA