Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waliouawa Gaza ni wengi kuliko miaka 4 ya vita duniani

Watoto waliouawa Gaza ni wengi kuliko miaka 4 ya vita duniani

Pakua

Wakati kukiwa na ripoti za mashambulizi kwa njia ya anga yanayotekelezwa na Israel huko Gaza usiku wa kuamkia leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA limesema idadi ya watoto waliouawa katika miezi ya hivi karibuni ni kubwa kuliko miaka minne ya mizozo duniani. 

Phillipe Lazzarini ambaye ni Mkuu wa shirika hilo la msaada kwa wakimbizi wa kipalestina hii leo kupitia mtandao wake wa X zamani Twitter ameandika ujumbe alioambatanisha na mchoro unaoonesha mambo mamwili kushoto kwenye rangi ya buluu idadi ya watoto waliouawa kutokana na vita tangu mwaka 2019 mpaka 2022 ambao ni 12, 193 na kulia ni idadi ya watoto waliouawa Gaza tangu mwezi Oktoba mwaka jana 2023 mpaka mwezi Februari 2024 ambao ni zaidi ya 12,300. 

Na ndipo akaandika ujumbe kuwa “Vita hii ni vita dhidi ya watoto. Ni vita dhidi ya utoto wao na mustakabali wao.”

Mkuu huyo wa UNRWA akaendelea na ujumbe wake na kusema kuwa “Sitisheni mapigano sasa kwa ajili ya watoto wa Gaza“.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka mamlaka za afya huko Gaza, mpaka sasa zaidi ya wapalestina 31,184 wameuawa na wengine 72,889 kujeruhiwa. 

Mpaka kufikia tarehe 12 ya mwezi huu wa Machi, wanajeshi 247 wa Israel wameripotiwa kuuawa na wengine 1,475 kujeruhiwa tangu kuanza kwa operesheni za ardhini kwa mujibu wa takwimu za jeshi la Israel. 

Sio mashambulizi tu ya mabomu yanayo gharimu maisha ya watoto na wakazi wa Gaza, janga la njaa nalo pia lipo hatihati kukumba wananchi hao ambao a misaada ya kibiandamu kuwafikia imekuwa changamoto kubwa. 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kibinadamu yamekuwa yakirejea kutoa maonyo kuhusu hali mbaya ya Gaza ambapo mtu mmoja kati ya wanne anakaribia kukumbwa na njaa. 

Mpaka sasa takriban watu 25 wamekufa kutokana na utapiamlo mkali na upungufu wa maji mwilini kaskazini mwa Gaza kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada, OCHA, 21 kati yao wakiripotiwa kuwa watoto.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limeonya kuwa vijana ni miongoni mwa wale ambao hawawezi kustahimili njaa na magonjwa, huku vijana milioni moja wakiwa tayari wameondolewa makwao kutokana na vita, na watoto 17,000 wasio na wasindikizaji au waliotenganishwa nao sawa na 1% ya watu milioni 1.7 ya wananchi wa Gaza wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Juhudi za ushirikiano wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kusaidia kupunguza hali hiyo ya kukatisha tamaa zinaendelea na hapo jana Shirika lake la Mpango wa Chakula Duniani WFP lilifanikiwa kufikisha Msaada mjini Gaza ambapo hawakuwahi kufika tangu tarehe 20 Februari.

Shirika jingine la UN lile la Afya WHO na wadau wake nao walifanikiwa kufikia hospital mbili zilizoko Gaza Kaskazini Al Shifa na Al Helo una kufikisha misaada ya vifaa tiba pamoja na mafuta ya kuendeshea mitambo ya hospitali. 

Hata hivyo mkuu wa shirika hilo la WHO Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia mtandao wa X alisema kuwa Hospitali ya  Al Shifa ilikuwa na inafanya kazi sehemu ndogo tu na inahitaji haraka wafanyakazi maalum wa afya.

Mahitaji yanasalia kuwa makubwa na ya haraka katika hospitali ya Al Helou, Dkt. Tedros aliongeza, huku huduma zikiwa chache katika idara zote, pamoja na uhaba wa mafuta, chakula, vifaa vya upasuaji na wafanyikazi wa matibabu.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'48"
Photo Credit
© UNICEF/Omar Al-Qattaa