Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Si haki kutumia gesi ya Nitrojeni Hypoxia kumuua Kenneth - Wasema wataalam wa UN

Si haki kutumia gesi ya Nitrojeni Hypoxia kumuua Kenneth - Wasema wataalam wa UN

Pakua

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akiwemo Alice Jill Edwards, anayeshughulikia masuala yanayohusu mateso, na Adhabu nyingine za Kikatili, za kinyume cha utu au za Kushusha hadhi, leo Januari 3 mjini Geneva-Uswisi wameelezea wasiwasi wao kuhusu kukaribia kutekelezwa kwa hukumu ya kifo kwa kutumia gesi ya nitrojeni hypoxia dhidi ya Kenneth Eugene Smith hapa nchini Marekani. Mwenzangu Anold Kayanda amekifuatilia kisa hicho kwa kina… 

ASSUMPTA: Anold hukumu ya kifo bado inatekelezwa katika maeneo kadha duniani, ni kwa nini hii ya sasa inafuatiliwa zaidi? 

ANOLD: Assumpta hilo ni swali muhimu hasa na jibu ni kuwa utekelezaji huu wa hukumu ya kifo umepangwa kufanyika kwa kutumia gesi ya Nitrojeni hypoxia ambapo huyu Kenneth Eugine Smith atanyimwa hewa ya Oksijeni lakini atapewa nafasi ya kuvuta hiyo gesi ambayo ndiyo itamuua. Sasa wataalamu hawa wa haki za binadamu wanasema kwa kuwa jambo hili halijawahi kujaribiwa  hapo awali, kwa hivyo utekelezaji unaweza kumfanya anayeuawa atendewe ukatili, unyama au udhalilishaji au hata kuteswa na kwamba hakuna ushahidi wa kisayansi wa kuthibitisha vinginevyo. 

ASSUMPTA: Nikikurudisha nyuma kidogo, huyu anayetarajiwa kuuawa kwa njia hii alifanya kosa gani? 

Smith alipatikana na hatia ya kuua kwa kukodiwa mwaka wa 1988 na kuhukumiwa kifungo cha maisha bila msamaha kwa kura 11 za kukubali na 1 ya kupinga. Hata hivyo, hakimu aliyetoa hukumu alipuuza pendekezo la jopo la mahakama la kifungo cha maisha na akamhukumu kifo. 

ASSUMPTA: Na mwisho ikiwa hukumu hii itatekelezwa, ni lini? 

ANOLD: Kenneth Smith, ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa kwa zaidi ya miaka thelathini, amepangwa kunyongwa Januari hii tarehe 25, 2024, katika Jimbo la Alabama hapa Marekani. Mamlaka huko Alabama hapo awali zilijaribu kumuua Smith mnamo Novemba mwaka juzi 2022 kwa kutumia sindano ya sumu, lakini jaribio hilo lilishindikana kwa hiyo na hili ni la kusubiri kuona.  

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Anold Kayanda
Audio Duration
2'1"
Photo Credit
© UNICEF/Josh Estey