Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu ni kusherehekea Umoja wetu katika tofauti zetu

UN: Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Binadamu ni kusherehekea Umoja wetu katika tofauti zetu

Pakua

DAFI, Mfuko wa Ufadhili wa Kimasomo kwa Wakimbizi, kwa kushirikiana na UNHCR wanawasaidia wakimbizi kutimiza ndoto zao za kupata elimu ya juu katika nchi ya kwanza wanakopata hifadhi baada ya kuzikimbia nchi zao. 

Idadi ya waliokwisha kunufaika na ufadhili wa DAFI inazidi kuongezeka lakini takwimu za hivi karibuni zinaonesha angalau hadi kufikia mwaka jana 2022 DAFI ilipotimiza miaka 30 tangu kuanziswa kwake, chini ya serikali ya Ujerumani na wadau wengine, tayari imewafadhili wakimbizi zaidi ya 24,000 kusoma elimu za juu iwe vyuo vikuu au vyuo vingine vya ujuzi.

Kwa leo tuchukue mfano mdogo tu wa nchini Rwanda. DAFI imewasaidia zaidi ya wanafunzi wakimbizi 500 tangu mwaka 2010 nchini humo. Wanafunzi 154 kati yao hivi sasa wanasoma katika ngazi ya chuo kikuu. Tuchukue wawili tu kuwawakilisha wengine mmoja anamalizia na mwingine ameshahitimu.

Eric Nshizirungu, mkimbizi kutoka DR Congo mkazi wa Kambi ya wakimbizi Kiziba nchini Rwanda yuko katika mwaka wake wa mwisho wa masomo akisoma Ufamasia katika Chuo Kikuu cha Rwanda, kampasi ya Remera, "Nia yangu katika masomo yanayohusiana na afya ni kwa sababu kadhaa kama vile kukulia katika kambi ya wakimbizi, kukabiliwa na changamoto nyingi ambapo afya inafunikwa na majanga mengine ya kibinadamu kama vile chakula, malazi na mengine. Kwa hiyo, niliendeleza azma hiyo kwamba siku moja hata kama sitafanikiwa nikiwa kambini, labda nitafanikiwa nikiwa sehemu nyingine, lakini nitaisaidia jamii katika masuala ya afya.”

Francois Mbyirukira, naye kutoka DRC, mkazi wa Kigali lakini mwenyeji wa Kambi ya wakimbizi ya Kigeme, kusini mwa Rwanda. Baada ya kuhitimu masomo, akaanzisha biashara yake ya samani: Viti, makochi, meza, masofa mazuri, vyote unapata kwake, “Nilichagua kusomea manunuzi kwa sababu yanaendana na kile ambacho nimekuwa nikifanya kuanzia zabuni hadi ugavi. Yote ni kuhusu kufanya biashara. Kwa maoni yangu, udhamini wa DAFI umefanya kazi kubwa sana. DAFI ilinijengea kujiamini. Leo ninafanya biashara mjini Kigali. Biashara yangu imepanuka sana.”

Naam hayo ni matunda ya wanadamu walio katika hali nzuri walioamua kushikamana na walio katika shida kama inavyokumbusha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Kibinadamu kuwa ni siku ya kusherehekea umoja wetu katika utofauti wetu. 

Mnamo mwaka 2005, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa azimio namba 60/209 lilitambua mshikamano kama moja ya tunu za kimsingi na za ulimwengu ambazo zinapaswa kuwa msingi wa uhusiano kati ya watu katika karne ya 21 na kwa maana hiyo Baraza likaamua kuitangaza tarehe 20 Desemba ya kila mwaka kuwa ya Mshikamano wa Binadamu.

Audio Credit
Anold Kayanda
Sauti
3'22"
Photo Credit
©UNDP/Julie Pudlowski